Uvinza FM
Uvinza FM
17 May 2025, 12:36 am

Wananchi watumieni maafisa maendeleo jamii dawati la msaada wa kisheria kupata elimu ya kisheria ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima hasa migogoro ya ardhi na mirathi.
Na Linda Dismas
Ikiwa leo ni siku ya pili ya muendelezo wa elimu juu ya mkopo wa asilimia kumi wa Mama Samia, maafisa maendeleo jamii dawati la msaada wa kisheria wilaya ya Uvinza hii leo wamewapatia elimu ya mirathi wajasiriamali hao.

Akizungumza na Uvinza fm radio Bi.Janeth Mwakibete amesema kuwa wanashirikiana na jeshi la polisi katika kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi wasio kuwa na elimu hiyo na hata wale ambao wanayo lakini bado wamepoteza haki zao za msingi.
Bi.Janeth ameendelea kwa kusema dawati la msaada wa kisheria limekuwa likihakikisha wanaifikia jamii kila mara ili kutambua changamoto zinazowakumba.
Aidha ameeleza kuwa wamekuwa wakipokea kesi za mara kwa mara zinazotokana na ukatili wa kijinsia hususani kwa kina mama na watoto na hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuripoti matukio hayo ili kupata msaada wa kisheria wa haki zao.
Nao baadhi ya wajasiriamali katika mafunzo hayo wameeleza namna walivyonufaika na elimu hiyo ya mirathi na kuwasihi wananchi wengine wawe na mazoea ya kujitokeza katika mafunzo mbalimbali yanayotolewa na serikali ili kuwasaidia kutambua haki zao za msingi.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa lengo la elimu ya mirathi ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya msingi.