

14 February 2025, 9:26 am
Serikali imeendelea kusisitiza suala la ulaji wa vyakula vyenye lishe bora kwa wazazi na watoto.
Na Theresia Damas
Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imefanya tathmini ya kikao kuangazia lishe bora ikiwa na maazimio mbalimbali ikiwemo watoto kula shuleni ili kuwajenga kimwili na kiakili pia.
Akiendesha kikao hicho Afisa Lishe Dismas Pokela amesema viashiria ambavyo vimeonekana bado utekelezaji wake uko chini kwa asilimia 33.4 jambo ambalo ni hatari kwani watoto kutokula chakula shule inapelekea udhaifu wa mwili na kunyemelewa wa magonjwa ikiwemo kupungukiwa na damu.
Afisa Lishe huyo ameendelea na kusema jamii ijenge tabia ya kula vyakula vyenye virutubisho vya kujenga afya na kuweka mkazo kwa watoto kupata lishe shuleni ili kutokomeza utoro na kujenga afya imara.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza Ndg. Acland Kambili ambaye amesimamia kikao hicho amewataka wananchi na watumishi wa afya waliohudhuria katika kikao hicho wakawe mabalozi kwa kutoa elimu kwa jamii huku akiomba wazazi wawe mstari mbele kuwapa watoto chakula lishe.