Serikali yaruhusu sekta binafsi kuanzisha safari za treni reli ya mwendokasi
7 December 2023, 3:33 pm
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa usafirishaji jijini Arusha. Picha na Anthony Masai
“Sheria ya reli namba 17 imefanyiwa marekebisho ambapo kwa sasa inaruhusu uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu ya reli“.
Na Anthony Masai
Serikali imeruhusu rasmi wadau wa sekta binafsi kuingia katika uwekezaji wa usafiri wa treni na kuitumia reli ya kisasa maarufu kama Standard Gauge ambayo kwa safari za Dar es Salaam hadi Morogoro zinatarajia kuanza mwezi Januari mwakani.
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa usafirishaji nchini kinachoendelea jijjini Arusha.
Prof. Mbarawa amesema serikali imeshafanya mabadiliko ya sheria ya reli namba 17 ambayo kwa sasa inaruhusu sekta binafsi kuja na vichwa na mabehewa yao na kutumia kwenye mfumo wa reli ya kisasa nchini.
Amesema awamu ya pili ya ujenzi wa reli hiyo kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma imefikia asilimia 95.7 na awamu ya tatu kutoka Makutupora hadi Tabora ujenzi wake umefikia asilimia 12.2, Tabora-Isaka asilimia 5.15 na Isaka-Mwanza asilimia 44.22.