PM Majaliwa: Madereva mnalogana?
20 August 2024, 9:59 pm
Na Joel Headman
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshtushwa na madai ya madereva wa Serikali kulogana ili wapate magari ya kufanyia kazi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Juma Mtanda kwenye kongamano la tatu la madereva wa serikali la mwaka 2024 linaloendelea jijini Arusha kwa siku nne mfululizo.
Mtanda amesema baadhi ya madereva wamekuwa wakilogana ili wapate magari ya kuendesha kutokana na vyombo vyao kuharibika na kuishia kukaa kwenye ajira wakilipwa mishahara bila kupangiwa majukumu, hivyo baadhi hufanya mambo hayo wapangiwe kazi.
Akizungumzia leo Agosti 20, 2024, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakuu wote wa taasisi na waajiri kuhakikisha wanafanya tathmini ya magari yote ya serikali yaliyoharibika na yatengenezwe, kuhakikisha madereva wote walioajiriwa wanapata vyombo vya kufanyia kazi.
“Mmh! hili la kulogana limenishtua sana, sijawahi kujua kwamba madereva mnafikia hatua ya kulogana ili mpate vyombo vya kufanyia kazi.”
“Hivyo sasa nitumie nafasi hii, kuwaagiza wakuu wote wa taasisi na waajiri waanze kufanya tathmini mapema sana ya kufufua magari ya serikali yaliyoharibika ili madereva wapangiwe kazi wasilogane kugombea machache yaliyopo,” amesema.
Mbali na hilo, amewataka waajiri kubainisha madereva waliopo kwenye taasisi zao ambao hawana vyombo vya kufanyia kazi au hawajapangiwa majukumu, ili serikali iwatambue na kuwapangia kazi.