Serikali: Hali ya umeme nchini yaanza kuimarika
31 January 2024, 7:09 pm
“Yalikuwa ni maelekezo ya mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha umeme unaimarika katika kipindi cha miezi sita”
Na. Anthony Masai
Serikali imesema hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme nchini inaendelea kuimarika licha ya kuwepo kwa upungufu wa nishati hiyo kwa baadhi ya maeneo na kwamba agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa TANESCO kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana ifikapo mwezi Machi 2024 litatekelezeka.
Kamishna wa umeme na nishati jadidifu wa Wizara ya Nishati anayesimamia umeme nchini Mhandisi Innocent Luoga amesema hayo katika mkutano wa kimataifa wa maendeleo ya nishati uliowakutanisha wadau wa sekta hiyo kutoka nchini mbalimbali Afrika unaoendelea jijini Arusha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Mhandisi Gisima Nyamhanga,amewataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati masuala ya nishati ya umeme yakiendelea kushughulikiwa.
Mkutano huu unatajwa kwenda kutatua changamoto za nishati ya umeme Afrika kwa kejenga ushirikiano katika maeneo ya uzalishaji na usambazaji.