Wafanyabiashara Babati walalamika kuondolewa kwa vibanda vyao
10 January 2025, 5:12 pm
Wajasiriamali wanaofanya shughuli zao katika hifadhi ya eneo la barabara kuu mjini Babati mkoani Manyara wamesema serikali ingewashirikisha na kuwapa mda wa kutafuta maeneo mengine kabla ya kuwaondoa kwenye maeneo hayo.
Na George Agustino
Kufuatia zoezi la kuwaondosha wajasiriamali wanaofanya shughuli zao katika hifadhi ya eneo la barabara kuu mjini Babati mkoani Manyara wajasiriamali hao wamesema serikali ingewashirikisha na kuwapa mda wa kutafuta maeneo mengine kabla ya kuwaondoa kwenye maeneo hayo.
Wakizungumza na fm Manyara leo baadhi ya wajasiriamali hao wamesema biashara walizokuwa wanafanya kando ya barabara ndio kazi pekee wanazotegemea kuwaingiza kipato cha kujikimu kimaisha na wanapoondolewa bila kupewa muda wa kujiandaa wala kuonyeshwa eneo mbadala watashindwa hata kupeleka watoto shule na kurejesha mikopo waliyochukua kwaajili ya biashara.
Aidha, fm Manyara imezungumza na mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati Shaban Mpendu amesema taarifa za kuwaondoa wafanyabiashara hao zimetolewa mapema na utaratibu wa kuwaondoa wafanyabiashara wote kando ya barabara ni zoezi endelevu na kwa mfanyabiashara anayehitaji eneo la kufanyia biashara anatakiwa kumfuata afisa biashara ili aelekezwe sehemu sahihi ya kufanyia biashara yake.