Adhana FM

Wanaokusudia kwenda hija wahimizwa kukamilisha taratibu kabla ya Februari 14, 2025

24 October 2024, 10:51 pm

Na Mwandishi wetu

Umoja wa taasisi za kusafirisha mahujaji Zanzibar UTAHIZA, umetoa taarifa kwa waislamu wanaokusudia kwenda kutekeleza ibada ya hija ya mwaka 1446/2025 kuwa mwezi 25 shaaban 1446 hijiria ni mwisho wa kusajili mahujaji katika mfumo wa hija inayofuata.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa UTAHIZA, Ustadhi Ali Adam amesema kuwa katika mwezi wa September mwaka huu, serikali ya Saudia Arabia imefanya mikutano ya maandalizi ya hija kwa njia ya mtandao, kwa mashirika yanayotarajia kusafirisha mahijaji mwaka huu ili kutoa fursa kwa mashirika ya hija kuanza taratibu za kuwasajili mahujaji.

Ustadhi Ali Adam amesema kuwa serikali ya Saudi Arabia imefanya mabadiliko katika taratibu za mfumo wa usajili wa mahujaji ambapo Zanzibar imetakiwa kuwa na mashirika manne yatakayotambuliwa na serikali ya Saudia Arabia na kila shirika kutakiwa kusafirisha angalahu mahujaji 500 kwa uchache.

Amesema kuwa pamoja na kuwa Tanzania imepewa nafasi 25,000 za kupeleka mahujaji nchini Saudi Arabia lakini kwa mwaka huu inatajariwa kuwasafirisha mahujaji 3600 ambapo Zanzibar itakua na mahujaji 2300 na Tanzania bara kuwa na mhujaji 1300. Aidha kutokana na utaratibu huo, mashirika ya kusafirisha mahujaji yatatakiwa kuungana kwa kuwa kwa Zanzibar hakuna shirika mabalo limewahi kutimiza idadi ya mahujaji inayotakiwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na wizara ya hija ya Saudia.

Akitoa maoni katika mkutano huo, Sheikh Faridi Hadi Ahmed amesema kuwa waislamu wanaokusudia kutekeleza ibada hiyo au kuwasaidia wazee wao wafanye hima kufuata taratibu mapema ili kuepuka usumbufu.

Naye Biubwa Othman, amesema kuwa Wakfu na mali ya amana Zanzibar imeazisha mfuko wa hija ambao unahitaji wanachama kujiunga na kuweka fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kwenda kutimiza nguzo ya hija huko Makkah,

Biubwa amesema kuwa Wakfu na mali ya amana imeweka utaratibu huo ili kuwarahisishia watu kuweka amana fedha zao kwa lengo la kwenda hija ambapo mfuko umeweka utaratibu wa aina tatu za wanachama kama vile mtu binafsi, mwanachama mweza na kikundi.

Amesema kuwa, Wakfu imeazisha mfuko wa hija kwa lengo la kuwa na mahujaji wengi wa Tanzania kwa kuwa hadi sasa idadi watu wanaotakiwa kwenda hija iliyowekwa na serikali ya Saudi Arabia haijafikiwa hivyo mfuko huo utakua ni fursa ya uhamasishaji watu.