Adhana FM

Mahujaji waliosafiri na Jumuiya ya Istiqama wawasili Minna kwa ibada

14 June 2024, 10:29 am

Na Waandishi wetu, Saudi Arabia na Zanzibar

Jumla ya mahujaji 104 waliosafiri na Jumuiya ya kusafirisha mahujaji ya Istiqama Zanzibar, wamewasili katika Mji wa Minna leo asubuhi.

Akitoa taarifa hiyo, Sheikh Sultan Khamis Al Mazrui, Mwenyekiti wa kamati ya hijja Istiqama Zanzibar amesema kuwa mahujaji wote wana afya njema na wanaendelea na ibada mbali mbali.

Sheikh Sultan amesema kuwa, mahujaji hao watakaa hapo leo na kufanya ibada mbali mbali hadi kesho wataposimama katika viwanja vya Arafa kwa ajili ya kukamilisha nguzo kuu ya hijja.

Sheikh Sultan amesema kuwa siku ya mwezi 8 Dhulhija imeitwa Yawmul Tarwiya kwa sababu watu walikua wakikusanya maji kwa ajili ya kuwanywesha mahujaji.

Nao baadhi ya mahujaji waliofanyiwa mahojiano na mwandishi wetu huko Makka wamesema kuwa wanafurahia maandalizi yaliyofanywa na Jumuiya pamoja na huduma wanazopata huko.

Wakati mahujaji hao wanatekeleka ibada ya hijja ambayo ni nguzo ya tano ya uislamu, waislamu duniani wapo kwenye siku 10 bora kwa mujibu wa Quran tukufu kama zilivyotajwa kwenye Surat Fajir.