Pen America lawafunza waandishi wa habari wanawake Zanzibar kujilinda na udhalilishaji wa kimtandao
20 December 2023, 8:09 pm
Na Najjat Omar-Zanzibar
Waandishi wa habari wanawake waliopo kwenye taasis mbalimbali za binafsi na Serikali wamekutanishwa pamoja na Shirikia na Pen America kwenye kikao cha siku mbili kilichojadili masuala ya udhalilishaji wa kimtandao,kulinda ,kujitetea na kuzingatia afya ya akili kwa waandishi hao.
Akifungua kikao hicho Mkufunzi na Mwandishi wa Habari kutoka nchini Kenya Cecilian Maundu amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa fursa ya elimu jumuishi kwa waandishi wa habari wanawake kujua na kulinda masuala ya taarifa binafsi na udhalilishaji wa kijinsia “ Ni tofauti sana kwa waandishi wanaume ,waandishi wanawake mara nyingi hupitia udhalilishaji mtandaoni wa binafsi na sio wa kikazi jambo ambalo linawanyima waandishi wanawake fursa ya matumizi ya mtandao kwa uhuru wa fani yao ” Amesema Cecilian.
Wakichangia mafunzo hayo baadhi ya washiriki akiwemo Khairat Haji kutoka Chama cha Waandishi wa habari wanawake – TAMWA – Zanzibar amesema udhalilishaji wa kimtandao ambao unawakuta waandishi wanawake ni jambo linalotokea mara kadhaa na kwa sababu ya kutojua ni kama wanawake wameanza kuona hali hio ni ya kawaida “Unaweka habari yako kwenye huo mitandao ila waokuja kuchangia pale ni watu ambao wataanza kukudhihaki kuhusu muonekana wako au maumbile yako jambo ambalo sio sahihi” Amemaliza Khairat.
Sheria ya masuala ya Usalama wa Mtandao ya mwaka 2015 inawalinda watumiaji wote wa mtandano juu ya udhalilishaji ila bado vitendo vya udhalilishaji wa waandishi wa habari wanawake vinaendelea.
Amina Mchezo kutoka radio Coconut na Maryam Juma kutoka Zanzibar leo Pemba ambao pia wameshiriki wamesema kwa pamoja hali ya udhalilishaji uliopo kwenye mitandao kuhusu kazi za waandishi wanawake mda mwengine zinaendelea hadi kwenye maisha ya kawaida kwa kuulizwa kwa nini umeandika taarifa ile jambo ambao sio sahihi “ Ukishaanzwa kuulizwa na jamii inayokuzunguka juu ya kuandika taarifa ile basi unaanza kukosa amani ya kuendelea kuweka kazi zako mtandao” Amesema Maryam alipokuwa akichangia.
Kikao hicho kilijikita zaidi juu ya usalama wa afya ya akili,matumizi sahihi ya mtandao,kujilinda na kupata msaada wa usalama wa matumizi ya mtandao pale udhalilishaji unapotokea.