Uvinza FM

Watumishi sita wa afya wafa maji Kigoma

13 March 2026, 6:05 pm

Picha ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro akiwa katika tukio la ajali. Picha na Abdunuru Shafii

watu sita wamethibitika kufariki dunia na miili yao imepatikana, huku watu wengine watatu waliokuwa kwenye boti hiyo wakiendelea kutafutwa na vikosi vya uokoaji kwa kushirikiana na wananchi

Na. Abdunuru Shafii

Watumishi sita wa Idara ya Afya kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma wamefariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama katika Ziwa Tanganyika karibu na kijiji cha Kalalangabo wilayani humo. Watumishi hao walikuwa wakielekea katika kijiji cha Kagunga kwa ajili ya kusambaza dawa pamoja na kutekeleza zoezi la utoaji chanjo na usajili wa Bima ya Afya kwa wote kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vya mwambao wa ziwa hilo.

Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamesema chombo hicho kilikumbwa na dhoruba kali iliyosababisha mawimbi makubwa kabla ya kupinduka na kuzama majini. Wamesema hali ya hewa ilibadilika ghafla na kusababisha upepo mkali pamoja na mawimbi yaliyofanya boti hiyo kushindwa kuhimili nguvu ya maji na hivyo kusababisha ajali hiyo kutokea.

sauti za baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Michael Maganga, amesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa mbili asubuhi katika kijiji cha Kalalangabo, Wilaya ya Kigoma, ndani ya Ziwa Tanganyika. Amesema watu sita wamethibitika kufariki dunia na miili yao imepatikana, huku watu wengine watatu waliokuwa kwenye boti hiyo wakiendelea kutafutwa na vikosi vya uokoaji kwa kushirikiana na wananchi. Aidha, ameeleza kuwa watu tisa waliokuwamo kwenye boti hiyo wameokolewa na kwa sasa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni.

sauti ya Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Michael Maganga

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa boti hiyo ilikumbwa na dhoruba kali kabla ya kupinduka na kuzama. Amesema watumishi hao walikuwa sehemu ya kundi la watu 18 waliokuwa ndani ya chombo hicho wakati wakitekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi katika maeneo ya mwambao wa ziwa.

Kwa mujibu wa Balozi Sirro, miili ya watumishi sita tayari imepatikana huku juhudi za kuwatafuta watu wengine watatu zikiendelea kufanywa kwa ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi. Aidha, ametoa wito kwa watumiaji wa usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika kuzingatia tahadhari na maelekezo yanayotolewa na mamlaka za hali ya hewa ili kupunguza hatari ya majanga kama hayo kujirudia.

sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro