Uvinza FM
Uvinza FM
5 February 2026, 4:23 pm

IDRAS ni mfumo jumuishi wa kodi za ndani unaolenga kumwezesha mlipakodi kupata huduma mbalimbali za kikodi akiwa katika eneo lake la biashara.
Na Abdunuru Shafii
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma imeendesha mafunzo kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Uvinza kuhusu utoaji wa huduma za kikodi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kupitia Mfumo wa IDRAS, unaolenga kurahisisha huduma na kuongeza ufanisi kwa walipakodi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa wa TRA Mkoa wa Kigoma kutoka Kitengo cha Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, Makilo Seuta Lukurunge, amesema mfumo wa IDRAS ni mfumo jumuishi wa kodi za ndani unaolenga kumwezesha mlipakodi kupata huduma mbalimbali za kikodi akiwa katika eneo lake la biashara bila ulazima wa kufika ofisini, hatua itakayorahisisha utoaji wa huduma kwa upande wa TRA na kuongeza ufanisi kwa walipakodi.
Makilo Seuta ameongeza kuwa mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika rasmi tarehe 09 Februari, 2026 ambapo walipakodi watanufaika kwa kupata huduma za kikodi kwa muda wote wa saa 24 siku saba za wiki, ikiwemo kuona madeni yao, kumbukumbu za miamala, risiti za manunuzi na mauzo pamoja na taarifa nyingine muhimu, huku TRA ikiendelea kutoa elimu kwa wadau ili kuhakikisha mfumo huo unaeleweka na kuchangia kuongeza mapato ya taifa.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Uvinza walioshiriki mafunzo hayo wamesema elimu waliyopata itawasaidia kurahisisha shughuli zao za biashara na kuondoa changamoto walizokuwa wakikumbana nazo awali, huku wakiiomba TRA kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara waliopo mijini na vijijini.
