Uvinza FM
Uvinza FM
27 September 2025, 10:15 pm

Nitashirikiana nanyi katika kuleta maendeleo yeti hapa Uvinza, kukamilisha barabara ya Karuele Hadi Shekeshe na kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa ardhi.
Na. Abdunuru Shafii
Mgombea udiwani wa Kata ya Uvinza kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Himidi Kisobwe, amefanya mkutano wa hadhara na kuwasilisha sera na vipaumbele vyake kwa wananchi na Huu ni mkutano wake wa kwanza tangu kuanza kwa harakati za kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wananchi wa maeneo mbalimbali, Kisobwe ameahidi kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanapatikana na kusema mshikamano kati ya kiongozi na wananchi ndio chachu ya maendeleo ya kweli katika jamii.

Miongoni mwa ahadi zake, ametaja kukamilika kwa barabara ya Karuele hadi Shekeshe kuwa ni kipaumbele chake kikuu na kusema barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, hivyo kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa mazao na huduma nyingine.
Aidha, Kisobwe ameweka wazi kuwa atafanya tafiti na kushughulikia changamoto ya upungufu wa ardhi katika Kata ya Uvinza na kuwa ardhi ipo, ila changamoto kubwa ni usimamizi na mgawanyo usio sahihi, jambo analodhamiria kulishughulikia kwa kushirikiana na wataalamu na wananchi.
Akihitimisha hotuba yake, mgombea udiwani wa Kata ya Uvinza kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Himidi Kisobwe amewaomba wananchi kumpa ridhaa kupitia sanduku la kura ili aweze kutekeleza ahadi na mipango aliyoiwasilisha na kusisitiza kuwa kura ya wananchi ndio msingi wa mabadiliko ya kweli na maendeleo endelevu kwa Kata ya Uvinza.