Kigoma: Serikali kuwachukulia hatua wazazi wasiowapeleka watoto shule
03/07/2023, 12:55 pm
Kutokana na wanafunzi kutojiunga na masomo ya sekondari na wengine kuchelewa kujiunga na masomo, serikali yaahidi kuendelea na zoezi la kuwakamata wazazi wanaokiuka amri hiyo kwa kutumia sheria mbalimbali
Na Glory Kusaga
Changamoto ya baadhi ya wazazi kutokuwa na mwamko wa kuwapeleka watoto wao shule imesababisha baadhi ya wanafunzi mkoani Kigoma kushindwa kuripoti shuleni baada ya kufaulu kwenda elimu ya sekondari
Akibainisha hali hiyo Afisa Elimu mkoani Kigoma Paulina Ndigeza amesema wapo baadhi ya wazazi ambao hawana mwamko wa kuwapeleka watoto shule na kuwapatia haki yao ya kielimu hivyo huwaficha wanafunzi hao.
Amesema halmashauri ambayo kuna utoro kwa asilimia kubwa ni halmashauri ya wilaya ya Buhigwe huku akikisitiza kuwa wataendelea na zoezi la kuwakamata kwa kutumia sheria mbalimbali kwa wazazi wote ambao wanachangia hali hiyo.
Mpaka kufungwa kwa dirisha la usajili Machi 31 mwaka huu mkoa wa Kigoma kwa wanafunzi waliofanikiwa kuendelea na shule ya sekondari walioripoti ni 40,738 huku idadi ya waliofaulu ilikuwa ni 44,090.