Tumbatu FM

Wanahabari ZNZ wanolewa kuripoti ukatili wa kijinsia katika siasa

18 June 2025, 2:50 pm

Pichani (aliesimama mbele) ni Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa akiendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari dhidi ya mbinu za kuriport matukio ya udhalilishaji. Picha na Vuai Juma na Juma Haji

“Wanawake wengi hukumbana na ukatili wa maneno, vitisho na hata kushambuliwa mitandaoni wanapojaribu kuwania nafasi za uongozi. Tunahitaji mabadiliko ya kimfumo na kijamii ili kuwalinda wanawake hawa na kuhakikisha wanashiriki siasa kwa usalama,” alisema Sizarina.

Na Abdul Sakaza

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Masuala ya Wanawake (UN Women), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania – Zanzibar (TAMWA-Zanzibar), wameendesha mafunzo ya siku moja juu ya namna ya kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake katika siasa.

Mafunzo hayo yamewakutanisha waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali Zanzibar na yalilenga kuwajenga uelewa na kuongeza juhudi za pamoja katika kupinga mifumo na vitendo vinavyowanyima wanawake nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uongozi na siasa.

Akizungumza katika mafunzo hayo, mwakilishi kutoka UN Women, Sizarina Hamis, alisema ukatili wa kijinsia unaowakumba wanawake wanasiasa unaathiri sio tu maendeleo yao binafsi bali pia maendeleo ya kisiasa na kijamii na taifa kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa, alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kutetea usawa wa kijinsia na kuon

doa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake katika siasa.

Khairat Haji, ni afisa kutoka TAMWA Zanzibar aliwataka wanahabari kushirikiana na asasi za kiraia kwa ukaribu zaidi katika kufuatilia, kuripoti na kuelimisha jamii kuhusu ukatili wa kijinsia, hasa unaolenga wanawake katika uongozi.

Baada ya kushiriki mafunzo hayo  waandishi wa habari waliohudhuria wameeleza kuguswa na kuhamasika zaidi kuchukua nafasi yao kama sauti ya mabadiliko   na wameahidi  katika uchaguzi wa  ujao kua sauti isiyoyumba kwa wanawake  wagombea . 

Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa mijadala na maazimio ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na mashirika ya haki za wanawake, huku ikisisitizwa kuwa mabadiliko hayawezi kufikiwa bila ushiriki wa makundi yote ya kijamii.