Tumbatu FM
Tumbatu FM
13 June 2025, 12:14 pm

Picha ya katibu tawala wilaya ya Kaskazini Unguja (alievalia nguo nyeupe) akikabidhi majiko ya gesi kwa wajasiriamali Mkoa wa kaskaIni Unguja.
Picha na Juma Haji
“Ujio wa majiko ya gesi utalinda afya za akina mama wakiwa katika shughuli za ujasiriamali pamoja na kuendeleza utunzaji wa mazingira”
Na Juma Haji
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kushirikiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, wametekeleza kwa vitendo ahadi ya waliyoiweka ya kutoa majiko ya gesi kwa wanawake wajasiriamali wadogo wadogo waliopo katika kijiji cha Kilindi, Jimbo la Nungwi, Wilaya ya kaskazini “A’’ Unguja.
Akikabidhi majiko hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja BiMariam Said Khamisi, amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia sera yake ya matumizi ya nishati safi kwa Watanzania.
Amesema iwapo wajasiriamali watayatumia majiko hayo wataliwezesha taifa kutoathirika na athari za mabadiliko ya tabianch kwani wajasiriamali wengi wamekua na tabia ya kutumia nishati ya kuni jambo linalopelekea uharibifu wa mazingira.
Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali, Bi. Helta Eliaus Salum ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, UWT na DAS kwa msaada huo.
Amesema wamekuwa wakisumbuliwa mara kwa mara na matatizo ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni, hivyo ujio wa majiko ya gesi utawawezesha kulinda afya zao wakiwa katika shughuli zao za kujitafutia rizk.
Aidha, ametoa ombi kwa serikali na wadau kuendelea kuwasaidia wanawake wajasiriamali katika fursa mbalimbali ili waweze kujiimarisha zaidi kiuchumi.