Ruangwa FM
Ruangwa FM
18 June 2025, 2:00 pm

Mkulima kijana kutoka Kijiji cha Mbangala, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Omari Said Jimajima (28), amefariki dunia baada ya kunywa sumu ya kuua wadudu aina ya Ninja, inayotumika kwenye mashamba, tukio lililotokea kwa huzuni kubwa na kuacha maswali kwa familia na jamii.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa, marehemu alifikishwa hospitalini kwa matibabu baada ya kunywa sumu hiyo mnamo Juni 13, 2025 majira ya saa sita mchana akiwa katika shamba lake la ufuta lililopo Kijiji cha Nachiungo. Alifariki dunia siku iliyofuata, Juni 14, akiwa bado anapatiwa huduma ya dharura.
Ripoti ya uchunguzi wa kitabibu imeeleza kuwa kifo kilisababishwa na kushindwa kwa ini kufanya kazi baada ya kuathirika na sumu hiyo kali.
Taarifa zaidi kutoka kwa majirani na ndugu zinasema kuwa kabla ya tukio hilo, marehemu alikumbwa na mgogoro wa kifamilia uliomhusisha na mchumba wake aitwaye Fatuma, mkazi wa Kiwawa, Wilaya ya Lindi Vijijini, ambaye anadaiwa aliondoka nyumbani bila taarifa rasmi mnamo Juni 9, majira ya saa mbili usiku
Jeshi la Polisi mkoani Lindi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na limeeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hilo linaweza kuhusishwa na msongo wa mawazo unaotokana na migogoro ya kifamilia.
Mwili wa marehemu tayari umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi.