Ruangwa FM

SMAUJATA wilaya ya Ruangwa kuanza ziara za kata kwa kata

8 May 2025, 7:33 pm

SMAUJATA Wilaya ya Ruangwa kuanza Ziara ya Kata kwa Kata kuimarisha Elimu, Uhamasishaji na Maendeleo ya vijana katika jamii.

“tumeazimia kuongeza nguvu katika usajili wa wanachama wapya ambapo Mpango huu unalenga kuongeza idadi ya wanachama wa SMAUJATA na kuhakikisha kuwa vijana wengi zaidi wanajumuishwa katika shughuli za maendeleo ya kijamii na uhamasishaji wa haki na usawa”

Na Mwandishi wetu

Kikao kazi muhimu cha SMAUJATA Wilaya ya Ruangwa kimefanyika jana katika ofisi ya kata ya Nachingwea, ambapo masuala kadhaa muhimu ya maendeleo ya vijana, elimu na ustawi wa jamii yamejadiliwa. Kikao hicho kimeweka mkazo mkubwa katika mpango wa ziara ya kata kwa kata, ikiwa ni jitihada za kufikia jamii kwa karibu zaidi.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Smaujata wilaya ndg. Edward Mbaruku amesema Kwa mujibu wa maazimio ya kikao hicho, ziara rasmi ya kata kwa kata inaanza Ijumaa hii kwa kutembelea shule ya Ruangwa Girls ambako kutatolewa elimu kwa wanafunzi,baadae ziara hiyo itaendelea Kata ya Mandarawe kwa ziara ya kuzungumza na wanafunzi pamoja na wazazi ikiwa Lengo kuu ni kutoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, elimu kwa mtoto wa kike na hamasa ya ushiriki wa vijana katika maendeleo ya kijamii.

Aidha Kikao pia kimeazimia kuongeza nguvu katika usajili wa wanachama wapya ambapo Mpango huu unalenga kuongeza idadi ya wanachama wa SMAUJATA na kuhakikisha kuwa vijana wengi zaidi wanajumuishwa katika shughuli za maendeleo ya kijamii na uhamasishaji wa haki na usawa.

Ikumbukwe SMAUJATA ni kampeni ya kitaifa ya kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili kwa watoto nchini Tanzania iliyoanzishwa na Sospeter Mosewe Bulugu mwaka 2022 chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi MaalumuKampeni hulenga kupinga kila aina ya ukatili, ukiwemo ukatili dhidi ya watoto.