Wazazi mahiri wapunguza ukatili Manyara
12 September 2024, 6:07 pm
Halmashauri za wilaya mkoani Manyara zimetakiwa kutambua mchango unaotolewa na wazazi mahiri ambao wamesaidia kupunguza changamoto za ukatili kwenye maeneo mengi wanayofanyia kazi
Na Marino Kawishe
Wizara ya maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalumu imezitaka halmashauri za wilaya mkoani Manyara kupitia maafisa maendeleo kutambua mchango na juhudi zinazofanywa na wazazi mahari wanao pambana na ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
Naibu katibu mkuu wizara ya maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalumu Felista Mdemu ameyasema hayo kwenye ofisi za shirika la So they can Tanzania alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa wazazi mahiri kutoka kata za Galapo, Qash, Mamire na Endakiso, amesema mchango unaotolewa na wazazi mahiri umesaidia kupunguza changamoto za ukatili kwenye maeneo mengi wanayofanyia kazi.
kwa upande wake meneja mkazi wa shirika lisilo la kiserikali la So they can Tanzania Roselyne Mariki amesema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo wameibua wazazi mahiri 114 wanawake kwa wanaume ambao wanafanya kazi zakujitolea kupambana na ukatili kwenye kata nne za mradi na wametumia muda mwingi kusaidia kata hizo ambazo zilikuwa na changamoto kubwa ya unyanyasaji pamoja na ukatili kwa watoto.
Baadhi ya wawakilishi wa wazazi mahiri wamesema changamoto zinazowakabili kwa sasa ni kukosa ushirikiano kwa baadhi ya viongozi wa vijiji, pamoja na swala la rushwa ambalo linakwamisha watuhumiwa wa ukatili kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa ambao wanapatikana na makosa ya ukatili kwa jamii.