Wakulima Manyara watakiwa kujisajili kupata ruzuku ya mbolea na mbegu
8 January 2025, 2:00 pm
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA Kanda ya Kaskazini imewataka wananchi mkoani Manyara kujisaliji katika maeneo wanayofanya shughuli zao za kilimo ili kunufaika na ruzuku ya mbolea na mbegu ambazo zinatolewa na serikali.
Na Mzidalfa Zaid
Wakulima mkoani Manyara wametakiwa kujisajili katika maeneo wanayofanya shughuli zao za kilimo ili kunufaika na ruzuku ya mbolea na mbegu ambayo inatolewa na serikali na kufuata taratibu zote za usajili.
Wito huo umetolewa leo na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania TFRA kanda ya kaskazini Gothard Liampawe alipokuwa akizungumza na fm Manyara, amesema ili mkulima apate ruzuku ya mbolea na mbegu ni lazima ajisajili kwa kujiandikisha ambapo atapewa namba ya kuchukulia mbolea na mbegu.
Liampawe amesema Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea kanda ya kaskazini inaendelea kutekeleza zoezi la ukaguzi kwa wasambazaji na mawakala wa mbolea kuhakikisha wakati wowote wanafanya biashara kwa kuzingatia sheria ya mbolea Na 9 ya mwaka 2009 na kanuni za 2011 huku akisema TFRA kanda ya kaskazini imejipanga kuendeleza zoezi la uhamasishaji kwa wakulima na kutoa elimu ya matumizi ya vishikwambi kwa maafisa kilimo wa Halmashauri zote 32 za kanda hiyo ili wawasajili wakulima kupitia vishikwambi vilivyogaiwa na Serikali.
Aidha, Liampawe amesema TFRA haitasita kumchukulia hatua mfanyabiashara ,msambazaji, wakala yeyote anayejihusisha na mbolea au mbegu atakayekiuka sheria ya mbolea na mbegu na kusisitiza kuwa hakuna njia mbadala ya mkulima kupata ruzuku ya mbolea na mbegu pasipo kujisajili .
Kwa upande wake mwakilishi wa ruzuku wa TFRA mkoa wa manyara Mohamed Bakari amesema kwa sasa wakulima wamekuwa na muamko wa kujisajili kupata ruzuku ya mbolea na mbegu.