Adhana FM

Wajasiriamali wa kilindi wapewa majiko ya gesi ili kuongeza usalama wa mazingira ya kazi zao.

13 June 2025, 12:01 pm

Pichani, wa kwaza kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja Bibi Mariam Said Khamisi akikabidhi majiko kwa kina mama wajasiriamali wa Nungwi Wilaya ya kaskazini “A”.

Picha na Juma Haji.

“Ujio wa majiko ya gesi utalinda afya za akina mama wakiwa katika shughuli za ujasiriamali”

Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kushirikiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, wametekeleza kwa vitendo ahadi ya waliyoiweka ya kutoa majiko ya gesi kwa wanawake wajasiriamali wadogo wadogo waliopo katika kijiji cha Kilindi, Jimbo la Nungwi, Wilaya ya kaskazini “A’’ Unguja.
Akikabidhi majiko hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja Bibi Mariam Said Khamisi, amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia sera yake ya matumizi ya nishati safi kwa Watanzania.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu wa Sheha wa Nungwi, Khamis Kibata kwa niaba ya Sheha wa Kilindi, amesema kuwa kutokana na ongezeko la wajasiriamali wanawake katika shehia hiyo, msaada huo wa majiko utasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda afya na kuongeza usalama wa mazingira ya kazi zao.

Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali, Bi. Helta Eliaus Salum ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, UWT na DAS kwa msaada huo.

Amesema wamekuwa wakisumbuliwa mara kwa mara na matatizo ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni, hivyo ujio wa majiko ya gesi utawawezesha kulinda afya zao wakiwa katika shughuli zao za kujitafutia rizk.

Aidha, ametoa ombi kwa serikali na wadau kuendelea kuwasaidia wanawake wajasiriamali katika fursa mbalimbali ili waweze kujiimarisha zaidi kiuchumi.

 Amesisitiza kuwa wao kama wanawake wako tayari kujitokeza na kupiga kura za ndiyo kwa Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi mwezi Oktoba kwa lengo la kuwarudisha viongozi hao kwenye madaraka ili waweze kuwahudumia zaidi wananchi.