Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wajane Afrika kufanyika Zanzibar 2024
9 December 2023, 11:34 am
Na Najat Omar
Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wajane Afrika kufanyika Zanzibar 2024.
Zanzibar : Kwa mara ya kwanza Zanzibar itapokea ugeni wa nchi 54 katika Mkutano mkuu wa Umoja wa wajane Afrika ambao unatarajiwa kufanyika Zanzibar mwezi June kuanzia tarehe 20- 22,2024.
Akizungumza na waandishi wa habari Rais wa Umoja wa Wajane Afrika Hope Nswakwesi katika Ukumbi wa Ofisi ya THRDC iliyopo Kisauni Zanzibar, amesema nchi 54 zitashiriki kwenye mkutano huo mkubwa wa siku tatu ambao utawakutanisha washiriki wengi wakiwemo wake wa marais, mawaziri wa nchi hizo,viongozi wa taasis mbalimbali,wanasheria na wadau wa haki za binaadamu na masuala ya sera na sheria.” Mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi na viongozi wengi kutoka nchi hizo watahudhuria kuzungumza kwa pamoja dhana ya wajane na haki zao “ Amesema Hope.
Dkt Monica Mhoja ni Mwenyekiti wa Bodi ya Umoja wa Wajane Afrika amesema siku hizo tatu zitatoa nafasi ya kujadili na kuondoka na kauli moja kwenye masuala ya Sheria na sera,Haki na Wajibu pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wanawake ,watoto na wajane.
Tabia Maulid Mwita akiwa mwenyeji wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo amesema wageni kutoka nchi hizo 54 wanaokuja Zanzibar ni kushiriki mkutano huo lakini pia kutalii na kuitembelea Zanzibar “ Wageni watakuwa wengi na Zanzibar ikiwa mwenyeji kwenye hili basi kwetu ni fursa kubwa “ Alimalizia Tabia.