Tume ya Utangazaji Zanzibar yasitisha matangazo ya Adhana FM
7 September 2023, 1:50 pm
Ni Baada ya Masafa yake Kuingiliana Masafa ya Anga
Na Harith Subeit Zanzibar
Kituo cha Radio Adhana Fm kilichopo mtaa wa Rahaleo Zanzibar kimesitisha matangazo yake kupitia masafa ya 104.09 FM kutokana na masafa hayo kuingiliana na masafa ya mawasiliano ya ndege .
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mkurugenzi wa kituo hicho Ustadh Munir Ali Muhsin amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kupokea barua rasmi kutoka Tume ya Utangazaji Zanzibar iliyowataka kusitisha matangazo hayo hadi pale watakapofunga kifaa maalum kinachojulikana kwa jina la band pass filter kitachowafanya kutoingiliana na masafa yoyote.
Aidha mkurugenzi huyo amebainisha kuwa zaidi ya shilingi milioni sita zinahitajika kwa ajili ya ununuzi wa kifaa hicho nje ya nchi.
Amewaomba wahisani wadau wa radio adhana kwa jumla kutoa sadaka zao kuchangia kituo cha radio adhana popote walipo dunianu kupitia nambari za mpesa 0767528769 yenye usajili wa Said Suleiman Omar na 0713422626 yenye jina la usajili Munir Muhsin.
Mkurugenzi Munir amefafanua kuwa Tume ya Utangazaji imewaruhusu kurusha matangazo yao kwa kupunguza nguvu kutoka Watts 800 hadi 500 lakini bado tatizo la muingiliano limeendelea nakuamua kuzima tena matangazo hadi ufumbuzi mwengine utakapopatikana.
Kituo cha kiislam cha Radio Adhana Fm kinarusha matangazo yake katika maeneo ya Zanzibar,Dar-es-salaam,Tanga,Mkoa wa Pwani na maeneo mengine ya muambao wa bahari ya hindi.