Waislamu wahimizwa kusom Quran tukufu, kuwa mahiri katika taaluma mbalimbali
20 August 2023, 6:16 pm
Na Juma Haji Juma
Wakili mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shekh Saleh Mubaraq amewataka mashekh na walimu wa madrasa za Qurani nchini, kufundisha riwaya mbalimbali za usomaji wa Quran tukufu ili kuongeza kiwango cha ujuzi, umahiri, ufaulu wa taaluma ya Quran na kumridhisha Mwenyezi Mungu.
Akizungumza na radio Adhana FM mara baada ya kukamilika kwa mashindano ya kuhifadhi Quran tukufu huko skuli ya Maandalizi Saateni, wilaya ya Mjini, yaliyofadhiliwa na familia ya Khamis Ala’briy ameeleza kuwa lengo la mashindano hayo ni kuwahamasisha waislamu kujifunza taaluma za Quran, kuwakumbuka na kuwaombea dua wazee wa familia hiyo.
Amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na mashekh na walimu wa madrasa katika kuhifadhisha Quran tukufu ipo haja ya kufundisha riwaya zote za usomajii Quran ili kupata usahihi na umahiri wa wa kuisomesha Quran kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu.
Akizungumza kwa niaba ya waandaaji wa mashindano hayo, mratibu wa mashindano Ustadhi Yussuf Juma Omar amesema kuwa ni lazima waumini wamuelekee Allah (S.W) ili kupata tawfiq katika mambo yao pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu kuwapa nguvu wadau wote waliojitokeza kufanikisha mashindano hayo.
Nao baadhi ya wanafunzi wa madrasa hizo bibi Nuru Jabir na Mvita Kombo Haji wamesema upo umuhimu kwa watu wazima kufuatilia masomo ya dini ya kiislam hata kama wakiwa na umri mkubwa na wamefafanua kuwa watu wazima wamehamasika na kujifunza mambo mbalimbali ya dini ya kiislamu.
Katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na madrasa ya akina mama ya Rasikhuna na Markazi Slamiya zilizopo Chumbuni Bamita, jumla ya wanafunzi 23 wamezawadiwa zawadi mbalimbali katika mashindano hayo.