SMZ yapandisha bei ya karafuu Zanzibar
7 August 2023, 10:25 am
Karafuu ni zao kuu la biashara Zanzibar na sasa bei ya zao hilo imeongezwa ili kukuza kipato cha wakulima visiwani humo.
Na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepandisha bei ya karafuu kutoka shilingi 14,000 hadi shilingi 15,000 kwa kilo moja ya daraja la kwanza kwa mwaka 2023-2024.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na kufunguliwa kwa vituo vya kununulia karafuu kwa Unguja na Pemba katika ofisi za Wizara hiyo iliyopo Kinazini mjini Unguja.
Amesema kuwa Shirika la Biashara la Taifa limefungua vituo mbali mbali vya kuauzia karafuu kuanzia tarehe 3 mwezi huu Unguja na Pemba,hivyo amewataka wananachi kuuza karafuu zote katika Shirika hilo la Biashara la Taifa ZSTC.
Amefahamisha kuwa kwa hatua ya awali shirika limeanza kufungua kituo cha Saateni kwa Unguja na kwa upande wa Pemba watatumia Kituo cha Mkoani, Madungu na Bandarini Wete kuuzia zao hilo na kauahidi kuongeza kufungua Vituo vyengine kulingana na mahitaji.
Akizungumzia suala la malipo kwa wakulima wa zao hilo amesema shirika limejipanga kuwalipa wananchi hapohapo kwa mfumo wa Kielektroniki kupitia mifumo ya benki, mitandao ya simu na fedha taslimu kwa kiwango kidogo cha karafuu.
Akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya kupunguziwa kilo alisema shirika limejipanganga kununua mashine za kielektroniki za kupimia karafuu ili kuondosha malalamiko hayo na kuwataka Wananchi kuzingatia usafi wa karafuu kabla ya kuzipeleka Vituoni ili Kuepusha Usumbufu.
Hata hivyo Waziri Omar aliwaasa wananchi kuanika karafuu zao kwa kutumia majamvi ili kupata ubora na daraja la kwanza la karafuu.
Bei ya Karafuu imekuwa ikiongezeka kila baada ya muda kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya zao hilo duniani.