Walimu watakiwa kuchangamkia fursa zilizopo
6 October 2021, 8:15 am
Na mwandishi wetu
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya mafunzo ya amali Zanzibar mhandisi Bakari Ali Silima amewataka walimu kuzifahamu fursa zilizopo katika uchumi wa bluu ili kuwaelekeza vijana kufikia lengo la ukuaji wa uchumi nchini.
Akizungumza katika siku ya maadhimisho ya kitaifa ya walimu duniani huko Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Utalii Maruhubi,amesema ni vyema walimu kujua fursa zilizopo nchini hasa kupitia uchumi wa bluu pamoja na kuongeza nguvu kubwa katika Utoaji wa taaluma zao.
Aidha Mkurugenzi huyo amewataka vijana mbalimbali kuwa makini katika kuchangamkia fursa zinazotolewa na walimu hao ili kufikia malengo yao waliojiwekea.
Akiwasilisha mada ya Historia ya walimu mwalimu Daudi Ali kutoka Chama cha walimu Zanzibar amesema walimu wanapaswa kuthaminiwa katika jamii kutokana na msaada wanaotoa katika kuwaelimisha vijana nchini kwa kuwapatia taaluma bora.
Aidha wamesema bado kuna baadhi ya walimu wana mtazamo usio sahihi juu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Wakizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili walimu wengi wamesema kuwa ni pamoja na kutopata mafunzo ya elimu mjumuisho katika skuli zao,jambo ambalo linaleta usumbufu katika ufundishaji.
Siku Ya Mwalimu Duniani Huadhimishwa kila mwaka ifikapo Tarehe 5 Oktoba ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Walimu wenye moyo wa kuhuisha elimu”.