Uvinza FM

Kampeni ya ugawaji wa vyandarua bure ngazi ya kaya yaanza wilayani uvinza

14 March 2025, 3:00 pm

Kwenye picha ni mkuu wa wilaya ya Uvinza, katibu tawala, mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Uvinza na baadhi ya maafisa katika uzinduzi wa mafunzo ya utekelezaji wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua.(Picha Abdunuru Shafii)

Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza visa vya malaria, bado kuna changamoto ya baadhi ya wananchi hutumia dawa za Malaria bila kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Na Abdunuru Shafii

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imezindua kampeni ya ugawaji wa vyandarua kwa kaya bila malipo ili kupambana na ugonjwa wa malaria. Kampeini hii, inayosimamiwa na Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Malaria, inalenga kuhakikisha kila kaya inapata vyandarua ili kulinda wananchi dhidi ya mbu wanaosababisha malaria.

Katika uzinduzi wa mafunzo ya utekelezaji wa kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Bi. Dinnah Mathamani, Ambae amekuwa mgeni rasmi katika warsha hiyo amesema kuwa vyandarua vipatavyo laki mbili sitini na mbili elfu mia tatu thelathini na saba vitagaiwa katika Wilaya ya Uvinza.

Sauti ya mkuu wa wilaya Dinnah Mathamani

Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza visa vya malaria, bado kuna changamoto ya baadhi ya wananchi hutumia dawa za malaria bila kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya. Hali hii inasababisha usugu wa vimelea vya malaria dhidi ya dawa, jambo linalohatarisha mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya ugonjwa huo.

Sauti ya mkuu wa wilaya Dinnah Mathamani

Amesisitiza umuhimu wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua. Ameeleza kuwa licha ya jitihada kubwa zinazofanywa, bado changamoto kubwa ni matumizi mabaya ya vyandarua, ambapo baadhi ya watu hutumia kwa shughuli zisizokusudiwa badala ya kujikinga na mbu.

Sauti ya mkuu wa wilaya Dinnah Mathamani

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa malaria bado ni changamoto kubwa ya kiafya duniani, hasa barani Afrika. Kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka 2024, idadi ya wagonjwa wa malaria iliongezeka kwa milioni 11, kutoka wagonjwa milioni 249 mwaka 2022 hadi milioni 263 mwaka 2023. Tanzania pekee ilirekodi wagonjwa takribani 8,555,000. Vifo vilivyotokana na malaria vilipungua kutoka 608,000 mwaka 2022 hadi 597,000 mwaka 2023.

Afisa Mtendaji wa Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Malaria, Winfred Mwafongo(Picha Abdunuru Shafii)

Nae Afisa Mtendaji wa Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Malaria, Winfred Mwafongo, amesema kampeni hii inalenga kupunguza maambukizi ya malaria kwa kuhakikisha kila familia inapata kinga bora. Ameeleza kuwa vyandarua vinavyotolewa ni muhimu vitumike ipasavyo ili kufanikisha malengo ya kampeni.

Sauti ya afisa mtendani Bw. Winfred Mwafongo

Pia ameongeza na kusema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopo katika nafasi sita za juu kwa nchi zenye maambukizi ya ugonjwa wa malaria hivyo Wananchi wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika kampeni hii kwa kuhakikisha wanachukua vyandarua na kuvitumia ipasavyo.

Sauti ya afisa mtendani Bw. Winfred Mwafongo

Takwimu zinaonesha kuwa, licha ya kupungua kwa vifo vinavyosababishwa na malaria, bado kuna haja ya kuimarisha juhudi za kinga na matibabu ili kudhibiti ugonjwa huu na kuhakikisha kuwa malaria inapungua kwa kasi na hatimaye kutokomezwa kabisa.