Uvinza FM
Uvinza FM
23 October 2025, 10:00 am

“Sisi kama wasimamizi tunatamani Uchaguzi ufanyike kwa amani kwa kufata sheria na taratibu zote za uchaguzi kwa sababu kuna maisha baada ya uchaguzi na kila mmoja afanye yale yanayomuhusu kwa kuzingatia amani na utulivu.”
Na Theresia Damas
Katika mwendelezo wa serikali kutimiza takwa la kikatiba la uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais kupitia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, sheria inavitaka vyama vya siasa kuteua mawakala wake watakaosimama kwa ajili ya chama siku ya uchaguzi na kutekeleza majukumu yao kikamilifu kama ilivyoelekezwa na Tume.
Katika kutimiza agizo hilo kata ya Uvinza wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma imefanywa zoezi la kuwaapisha mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT – Wazalendo ili wakaitende kazi yao ya kisheria kwa uaminifu, bila vurugu wala ghasia yoyote ifikapo Octoba 29 .
Akizungumza na Uvinza FM baada ya zoezi hilo la kiapo kwa mawakala Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kata ya Uvinza Ndg. Antony Josephat amesema miongozo na maelekezo waliyoyatoa yamekamilika mawakala wameridhika, wamepata viapo na wamewasisitiza viongozi wa vyama vyao kuwafundisha kwa kina nini wanachopaswa kufanya siku ya uchaguzi.

Sauti ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kata ya Uvinza Ndg. Antony Josephat akizungumzia zoezi lilivyokuwa mara baada ya uapisho.
Antony ameongeza kwamba,” sisi kama wasimamizi tunatamani Uchaguzi ufanyike kwa amani kwa kufata sheria na taratibu zote za uchaguzi kwa sababu kuna maisha baada ya uchaguzi na kila mmoja afanye yale yanayomuhusu kwa kuzingatia amani na utulivu huku akiwasihi mawakala kufika kwa wakati na wapiga kura wajitokeze kupiga kura.”
Kwa upande wao mawakala wa CCM na ACT – Wazalendo wakiwakilishwa na Bi Tamasha Kheri wameishukuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwapata Elimu na kiapo kinachowapa nia na dhamira ya dhati ya kufanya kazi yao kwa moyo na kwa uhakika na kuwataka mawakala wengine wote Tanzania kufata Sheria za Uchaguzi na nchi kwa ujumla.