Uvinza FM

Vipigo kwa wanawake wajawazito hupelekea kuzaliwa kwa watoto njiti

8 July 2023, 10:14 pm

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka wanaume wenye tabia za kupiga wake zao wakati wakiwa wajawazito kuacha mara moja tabia hiyo.

Makamu wa Raisi Dr. Philip Mpango akikata utepe katika hafra ya kukabidhiwa vifaa vya kusaidia kukabili changamoto ya watoto njiti kwenye hospitali ya wilaya Buhigwe

Na. Abdunuru Shafii

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amepokea misaada mbalimbali iliyotolewa na taasisi ya Doris Mollel Foundation na Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) kwa ajili ya kusaidia kukabili changamoto ya watoto njiti kwenye hospitali ya wilaya Buhigwe mkoani Kigoma.

Amesema kuwa kila mwaka watoto zaidi ya 213,000 wanazaliwa kabla ya wakati na kati ya hao watoto 9,000 hufariki hii ni kutokana na magonjwa mbalimbali kwenye mfuko wa kizazi na kuwataka wanaume kuwa na tabia ya kuwasindikiza wake zao klinki ili kufahamu afya ya mama na mtoto.

Sauti ya Makamu wa Rais Dr. Philip Mpango akitoa takwimu

Dkt. Mpango ameongeza na kusema kuwa wapo wanaume wanaowapiga wake zao jambo linalochangia kuwapa akina mama wajawazito msongo wa mawazo na kupelekea kuzaliwa kwa watoto kabla ya wakati (watoto njiti) na kuwata wanaume wote nchini kuacha tabia hiyo mara moja na viongozi wa dini na viongozi wa serikali kutolifumbia macho swala hilo.

sauti ya Makamu wa raisi Dr. Philipo Mpango akikemea vipigo kwa wanawake

Naye Doris Mollel Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation amesema kuwa taasisi yake imekuwa ikisimamia na kuendesha taratibu ya kusaidia watoto njiti kutokana na changamoto kubwa inayowakabili wajawazito wanaoijifungua watoto hao na kufanya ukuaji na malezi yao kuwa na mashaka.

Doris Mollel Foundation wamekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 190 ikiwa ni sehemu ya kiasi cha shilingi bilioni 1.3 ambazo taasisi hiyo imetumia kwa ajili ya misaada ya mpango wa kusaidia watoto njiti toka ilipoanzishwa mwaka 2015.