Tumbatu FM
Tumbatu FM
20 July 2025, 9:36 am

“Ikiwa wakulima wanalima zao la mpunga watatumia mbegu zilizo bora wataweza kupata faida kubwa kwenye kilimo chao na kuondokana na umaskini“
Na Latifa Ali.
Wakulima wanaolima zao la mpunga wametakiwa kutumia mbegu bora ili kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji wao.
Wito huo umetolewa na mtafiti wa zao la mpunga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar (ZALIRI), Salum Faki Hamad, wakati wa hafla ya uvunaji wa mbegu kumi za majaribio iliyofanyika katika bonde la umwagiliaji maji Chaani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kuwa lengo la majaribio hayo ni kuchagua mbegu bora kati ya aina kumi, zikiwemo mbegu mpya pamoja na zile zilizotumika kwa muda mrefu, ili kubaini zile zitakazoongeza tija kwa wakulima na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa bonde la umwagiliaji maji Chaani, Ahmad Ali Juma, alisema kuwa zoezi la uvunaji wa mbegu hizo limewashirikisha wakuu wa vituo vya kilimo, mabwana na mabibi shamba, pamoja na wakulima wa bonde hilo nakuongeza kuwa baada ya uvunaji, sampuli zitachukuliwa na kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi na taasisi ya ZALIRI ili kubaini mbegu bora zinazokidhi mahitaji ya wakulima wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa mbegu tano bora zitakazopatikana katika majaribio haya zitaendelea kufanyiwa majaribio ya awamu ya pili msimu wa vuli, ambapo zitapandwa hadi hatua ya kuvunwa na hatimaye, mbegu mbili bora zaidi ndizo zitakazopendekezwa rasmi kwa matumizi ya wakulima katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Naye Meneja wa Mradi wa PMC FOR ODA Zanzibar, Francis Kim, alisema kuwa mradi huo umejikita katika kuwawezesha wakulima wa Zanzibar kwa kuwapatia mbegu bora, kuboresha miundombinu ya kilimo na kutoa mafunzo ya kuwawezesha kufanya kilimo cha kisasa chenye kuongeza kipato na kuimarisha maisha yao.