Tumbatu FM

Watendaji someni katiba sheria na kanuni ili kusimamia vyema sulala la uchaguzi

17 July 2025, 2:04 pm

Picha ni ni watendaji wa uchaguzi wakiwa kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu huko polisi Ziwani Zanzibar.Picha na Latifa Ali.

Iwapo vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa vitashirikishwa katika michakato yote ya uchaguzi kutachangia kwa kiasi kikubwa uchaguzi kuwa wa huru na wahaki

Na Latifa Ali.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaasa watendaji walioteuliwa kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Madiwani kwa Tanzania Bara kuhakikisha wanasoma na kuelewa kikamilifu Katiba, Sheria, Kanuni Taratibu na Miongozo ya Uchaguzi.

Wito huo umetolewa katika ufunguzi wa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk yaliyofanyika katika ukumbi wa Polisi Ziwani Zanzibar.

Amesema suala la uchaguzi ni mchakato wa kikatiba unaojumuisha hatua pamoja na taratibu za kisheria zinazopaswa kuzingatiwa kwa ufanisi, ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru wa haki.

Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria hali itakayo waepusha kuonekana ni cha malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi.

Hata hivyo amehimiza kihusu umuhimu wa kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum na kuweka mipango madhubuti itakayowezesha uchaguzi kufanyika kwa utulivu na usalama.

Amefafanua kuwa uteuzi wa watendaji hao umezingatia Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, na masharti ya Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inaipa Tume mamlaka ya kusimamia na kuratibu chaguzi hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ofisi ya Zanzibar, Ndugu Adam Juma Mkina, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watendaji hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata katiba, sheria na taratibu zote za uchaguzi.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamewahusisha waratibu wa uchaguzi ngazi ya mikoa, vyuo vya mafunzo, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao katika ngazi ya Majimbo