Tumbatu FM
Tumbatu FM
1 July 2025, 1:43 pm

“Wanawake wamekuwa msitari wa mbele kugombania nafasi za uongozi ndani ya mkoa wa kaskazini Unguja hali hii inatuonesha wazi kuwa mkoa wetu umepiga hatua kwenye demokrasia”
Na Vuai Juma
Chama cha mapinduzi mkoa wa Kaskazini Unguja kimesema kinatambua juhudi na michango ya viongozi wanawake katika kuliletea taifa maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na katibu wa umoja wa vijana chama hicho Moh’d Ali Moh’d wakati akizungumza na Radio Jamii Tumbatu huko ofisini kwake mahonda mkoa wa Kasakazini Unguja.
Amesema kwa mwaka huu wanawake wa CCM waliomo kwenye mkoa huo wamehamasika kwa wingi kuchukua fomu za kugombania nafasi za Uongozi kwenye siasa ikiwemo viti maalum kwa vijana kwa nafasi za uwakilishi ubunge na udiwani hali inayoonesha namna chama hicho kinavyowaunga mkono wanawake kwenye suala la demokrasia sambamba na kuwataka vijana kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu.

Kwaupande wake Amina Bakari Yussuf Mbunge viti maalum upande wa vijana mkoa Kaskazini Unguja amesema wanawake waliopata nafasi za kuongoza kwenye ngazi mbali mbali wamekuwa na mchango mkubwa kwenye taifa hili huku akiwataka wanawake vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kugombania nafasi za uongozi kwenye ngazi ya siasa Pamoja na kuendelea kuungamkono juhudi za serikali.
Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama cha mapinduzi (CCM) limeanza rasmi tarehe 28 Juni na linatarajiwa kufungwa mnamo tarehe 2 Julai mwaka huu.