Msaraka aridhishwa mradi wa ujenzi skuli ya Tumbatu
18 December 2024, 12:33 pm
Picha ya Mkuu wa Wilaya Kaskazini “A” (aliyevaa saa ya mkononi) akiwa pamoja na viongozi wengine wa wilaya wakiwa katika ukaguzi wa mradi wa shule ya Tumbatu.
Picha na Sheha Haji.
“Ikiwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati maeneo ya vijijini kutasaidia kupatikana kwa maemdeleo ya haraka”.
Na Sheha Haji.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja, Bw. Rashid Msaraka amesema ameridhishwa na Mradi wa Ujenzi wa Skuli ya Tumbatu.
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya mradi huo huko Wilaya Ndogo ya Tumbatu, Bw. Msaraka ameeleza kuwa utekelezaji mradi huo umefikia katika hatua nzuri hivyo amewataka Wasimamizi kuzidisha bidii ili waukamilishe Kwa wakati uliopangwa.
Kuhusu miradi mingine inayojengwa katika kisiwa cha Tumbatu, Bw. Msaraka amesema ujenzi wa miradi ya barabara na afya tayari umeanza, huku mradi wa bandari na uwanja wa mpira unatarajiwa kutekelezwa baada ya muda mfupi.
Naye Mhandisi Msaidizi katika ujenzi wa skuli hiyo, John Simon, amesema kumekuwa na changamoto katika usafirishaji wa vifaa vya ujenzi kutokana na mazingira ya kisiwa hicho kinachotegemea usafiri wa baharini.
Hata hivyo, amebainisha kuwa wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Mradi wa ujenzi wa skuli ya Tumbatu unatarajiwa kufunguliwa Disemba 31 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika shamrashamra za Sherehe za Mapinduzi Zanzibar.