Ruangwa FM

Lindi yatenga million 15 ujenzi matundu ya vyoo shule ya msingi Sinde

14 September 2024, 8:12 am

MANISPAA YA LINDI YATENGA MILIONI 15 UJENZI WA MATUNDU YA VYOO SHULE YA MSINGI SINDE .

NA HADIJA OMARY Lindi

Halmashauri ya Manispaa ya Lindi imeamua kutenga kiasi cha milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 8 ya vyoo katika shule ya msingi Sinde, iliyoko katika eneo hilo.

Hatua hii imechukuliwa baada ya miezi kadhaa ya malalamiko kutoka kwa wanafunzi na wananchi, ambao walionyesha wasiwasi kuhusu uhaba wa vyoo katika shule hiyo.

Shule ya Msingi Sinde ina jumla ya wanafunzi 316, kati yao wavulana 137 na wasichana 179. Ikijumuisha wanafunzi wa Madarasa ya Awali na lasaba Hata hivyo, shule hiyo ina matundu manne pekee ya vyoo, hali inayochangia ugumu wa huduma za afya na usafi kwa wanafunzi.

Hali hii imepelekea kutokidhi mahitaji ya msingi, hasa kwa watoto wadogo wa madarasa ya awali na la kwanza ambao wanaweza kuwa na hatari ya magonjwa kama vile minyoo na kuhara.

Kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tundu moja la choo linapaswa lihudumie wanafunzi 25 wa kiume na 20 wa kike. Hii inaashiria kuwa shule hiyo inahitaji matundu zaidi ili kutimiza viwango vinavyotakiwa.

Ujenzi wa matundu 8 mpya utaongeza idadi ya matundu ya vyoo hadi 12, lakini bado haitoshi kulingana na viwango vya mwongozo huo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele, amesema kuwa mradi huu utaanza mara moja, huku akiongeza kuwa ni hatua ya mwanzo tu katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo. Mnwele amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wananchi wakati wa utekelezaji wa mradi huu.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mnali, Yahaya Selemani, ameipongeza halmashauri kwa hatua hiyo, akisema kuwa wananchi tayari wameanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi.
Aidha, Mariam Saidi, mkazi wa mtaa wa Mnali, ameishukuru Serikali kwa kujali mahitaji ya wananchi na kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha hali hiyo.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Lindi, Joseph Mabeyo, ameeleza kuwa changamoto hii haipo kwenye shule ya msingi Sinde pekee bali ni tatizo linalowakumba shule nyingi katika mkoa huo.

Katika kikao cha wadau wa elimu, Mkuu wa Mkoa, Zainab Tellack, ameahidi kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha kuwa changamoto za miundombinu katika shule za msingi na sekondari zinatatuliwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Kitabu cha Basic Education Statistics for Tanzania (BEST) cha mwaka 2018, hali ya vyoo katika shule za msingi za Serikali ni mbaya, ambapo uwiano wa vyoo kwa wanafunzi ni mkubwa kuliko viwango vinavyotakiwa.

Hatua ya halmashauri ya Manispaa ya Lindi kutenga fedha hizi ni mwangaza wa matumaini kwa jamii, huku ikiashiria jitihada za kuboresha hali ya elimu na huduma za afya kwa wanafunzi.