Ruangwa FM
Ruangwa FM
26 August 2025, 5:08 pm

Ruangwa, Lindi – Agosti 26, 2025:
Mgombea mteule wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Ruangwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kaspar Kaspar Mmuya, leo amechukua fomu ya uteuzi katika ofisi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.
Akizungumza mara baada ya kupokea fomu katika ofisi za chama cha mapinduzi CCM Ruangwa Mmuya alisema amejiandaa kuendeleza juhudi za maendeleo zilizoanzishwa na Mbunge mstaafu Kassim Majaliwa, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayeondoka kwenye nafasi hiyo ya ubunge.
“Nitakuwa daraja kati ya wananchi na Serikali. Nitahakikisha changamoto zao zinafikishwa na kupatiwa majibu kupitia taasisi husika, huku nikifanya ziara kata kwa kata kusikiliza mahitaji ya watu wangu,” alisema Mmuya.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Bw. Mbesigwa alieleza kuwa taratibu zote za kisheria na kanuni za uchaguzi zimeambatanishwa na fomu hiyo, na wagombea wote wanatakiwa kuzifuata kwa ukamilifu ili kuhakikisha mchakato unakuwa huru na wa haki.
Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Ruangwa, Comrade Kasambe Hokororo, aliwaomba wananchi kumpa ushirikiano mgombea huyo kwa kuwa ana sifa stahiki za kuendeleza maendeleo ya jimbo hilo.
“Tumuunge mkono kijana wetu. Ni msikivu na pia ni msomi. Tunaamini ataendeleza pale tulipoishia,” alisema Hokororo.

Tukio hilo limehudhuriwa na wanachama wa CCM pamoja na wananchi waliomsindikiza kwa wingi, wakionesha hamasa zao.
Uchukuaji huo wa fomu ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu, ambapo vyama mbalimbali vinaendelea kuwasimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi