Ruangwa FM

Migogoro ya ardhi kupungua Ruangwa

25 July 2025, 12:59 pm

Mmoja wa wananchi wakiwa na mwongozo wa kumiliki Ardhi. Picha na Mtandao

Tusiangalie hati hizi kama karatasi tu, hizi ni nyenzo za maendeleo zitunzeni na msizitumie kama dhamana kwa mikopo isiyokuwa na tija bali mikopo yenye malengo ya kuinua maisha yenu na familia zenu.” DED Ruangwa Frank Chonya.

Na mwandishi wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Ndugu Frank Fabian Chonya amepongeza utoaji wa hati 1,243 za hakimiliki za kimila kwa wananchi wa vijiji vya Nambilanje na Namkatila kuwa ni hatua muhimu ya kumaliza migogoro ya ardhi hususan kati ya wakulima na wafugaji.

Katika maelezo yake siku ya Jumatatu tarehe 21 Julai 2025 wakati wa zoezi la kugawa hati hizo ambapo alikuwa mgeni rasmi Ndugu Chonya amesema kuwa wananchi wa Kijiji cha Nambilanje wamekabidhiwa hati 643 huku Kijiji cha Namkatila wakipokea hati 600 hatua inayotekelezwa chini ya mpango wa matumizi bora ya ardhi unaoratibiwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya aridhi.

Aidha amesema kuwa mpango huu umeleta suluhu ya kweli kwa changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikisababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha kila mwananchi anapata haki ya kumiliki ardhi kwa usalama na uhakika.

Vilevile ameweka bayana kuwa hati hizo za kimila zinatambulika kisheria na zinaongeza thamani ya ardhi kwa wamiliki wake pamoja na kuwapa fursa ya kuitumia kama dhamana kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kiuchumi hususan kilimo biashara na ufugaji wa kisasa.

Kwa kuzingatia umuhimu wa nyaraka hizo Mkurugenzi Chonya amewataka wananchi kuhakikisha wanazitunza kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa ni vielelezo rasmi vya umiliki wa ardhi na urithi wa kizazi kijacho

“Tusiangalie hati hizi kama karatasi tu hizi ni nyenzo za maendeleo Zitunzeni na msizitumie kama dhamana kwa mikopo isiyokuwa na tija bali mikopo yenye malengo ya kuinua maisha yenu na familia zenu” ameonya Mkurugenzi Chonya

Sambamba na hayo amewahimiza wananchi kuzingatia mipaka iliyoanishwa katika hati zaokuepuka uvamizi wa maeneo ya wengine.