Sekta ya madini ni nguzo kuu ya uchumi wa taifa – Dkt. Kiruswa
Sekta ya madini ni nguzo kuu ya uchumi wa taifa – Dkt. Kiruswa
13 June 2025, 10:04 pm
Watanzania watakiwa kuiona sekta ya madini kama dira ya maendeleo na fursa za mabadiliko ya kiuchumi
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ametoa wito kwa Watanzania kuipa kipaumbele sekta ya madini, akiielezea kuwa ni mhimili mkubwa unaochochea ustawi wa uchumi wa Taifa la Tanzania.
Akizungumza Juni 13, 2025, mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Lindi Mining Expo 2025, Dkt. Kiruswa alieleza kuwa mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa umeendelea kupanda kwa kasi, na kufikia zaidi ya asilimia 10.
“Sekta ya madini kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 10 ya pato la taifa. Kwa upande wa fedha za kigeni, tunazalisha zaidi ya dola bilioni 3 na tunakaribia kufikia bilioni 4,” alisema Dkt. Kiruswa.
Aidha, alifafanua kuwa mapato hayo yanatokana na kodi, ada mbalimbali, tozo, pamoja na ushiriki wa serikali katika baadhi ya migodi kupitia umiliki wa hisa.
mkuu wa wilaya ya kilwa Mohamed Nyundo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, aliipongeza Lindi kwa kuwa mwenyeji wa maonesho hayo akisema yamefungua milango ya fursa si tu kwa ukanda wa kusini, bali kwa taifa zima.
Katika maonesho hayo, kampuni ya Karunje, inayoendeshwa na wanawake wengi na kuongozwa na Mkurugenzi Kuruthumu Runje, ilionyesha jinsi wanawake wanavyoweza kung’ara katika sekta ya madini.
“Hii ni fursa ya kupanua soko letu na kujifunza matumizi ya madini katika mikoa mingine. Tumejifunza mengi kupitia maonesho haya,” alisema manager Kibibi kutoka Karunje.