Ruangwa FM
Ruangwa FM
11 June 2025, 10:02 pm

Na Loveness Joseph
Mkoa wa Lindi umeandika historia tena kwa kuzindua rasmi Maonesho ya Madini na Fursa za Kiuchumi 2025, tukio kubwa linalolenga kuhamasisha uwekezaji na kuibua fursa katika sekta ya madini kwa maendeleo ya kiuchumi ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Juni 11, 2025, ukiongozwa na mgeni rasmi Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Shaibu Hassani Kaduara, aliyemuwakilisha Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Antony Mavunde.
Akihutubia katika uzinduzi huo, Mhe. Kaduara alieleza kuwa sekta ya madini ina nafasi kubwa katika kuinua uchumi, hasa kwa mikoa yenye utajiri mkubwa wa rasilimali hiyo kama Lindi.
Kaduara alibainisha kuwa ongezeko la bei ya madini katika soko la kimataifa ni fursa ya kipekee kwa wachimbaji wadogo, wawekezaji na viwanda vinavyotegemea madini.
“Tukiimarisha mazingira ya uchimbaji, uwekezaji na uongezaji thamani madini, vijana wetu na wananchi kwa ujumla watanufaika zaidi na rasilimali zilizopo,” alisema Waziri Kaduara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainabu Telack, alieleza kuwa maonesho haya ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha wachimbaji wakubwa na wadogo, huku yakilenga kuhakikisha mkoa unanufaika kikamilifu na madini yake.
“Lengo ni kuwezesha Lindi kuwa kitovu cha uwekezaji wa madini kwa kutumia maonesho haya kama daraja la fursa na maarifa,” alisisitiza Mhe. Telack.
Mratibu wa maonesho hayo, Ndugu Mwinjuma Mkungu, alisema kuwa hii ni mara ya pili maonesho hayo kufanyika mkoani Lindi, baada ya mafanikio makubwa yaliyoshuhudiwa katika toleo la kwanza pia amesema kuwa mwaka huu, kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wachimbaji, wawekezaji na wadau wa madini, jambo linaloashiria kuimarika kwa sekta hiyo katika ukanda wa Kusini.
Maonesho haya ya siku nne yatafanyika kuanzia Juni 11 hadi Juni 14, 2025, yakihusisha maonyesho ya teknolojia, semina,kutoka kwa taasisi mbalimbali za sekta ya madini.