Ruangwa FM

Madiwani, wakuu wa idara Mtwara wajifunza uendeshaji wa ghala Ruangwa

14 December 2024, 8:16 pm

Ghala la Lipande halmashauri ya wilaya ya Ruangwa

Na Loveness Daniel.

Leo, 14 Desemba 2024, Baraza la Madiwani kutoka Kamati ya Uchumi na Fedha ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, pamoja na wakuu wa idara na vitengo, wamefanya ziara ya kujifunza namna ya uendeshaji wa ghala la ukusanyaji wa mazao katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ziara hii ililenga kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mazao na kuchochea mapato ya ndani.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Shadida Ndile, amesema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kukuza mapato ya ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani na kuimarisha maendeleo ya nchi kwa kutumia mifumo bora ya ukusanyaji wa mazao pia amesisitiza umuhimu wa kuhamasisha wananchi katika ukusanyaji bora wa mazao kwa kupitia mifumo ya kisasa.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Nolasco Kilumile, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo, alieleza kuwa ghala la Ruangwa limegharimu zaidi ya bilioni 5.7, fedha ambazo zilitolewa na serikali kuu kupitia ruzuku maalumu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwa mradi huu ulimalizika katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Kilumile alibainisha kuwa ghala linaendeshwa kwa mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ambapo Wilaya ya Ruangwa ina vyama vya ushirika 32 ikiwa vyama vya msingi ni 27 na wakulima 8,624 walioungana katika vyama hivyo akitaja mfumo huu ni mfumo unaosaidia wakulima kuuza mazao yao kwa urahisi, huku wakipata bei bora.