Kahama FM

Mbunge Kishimba ashauri mazao mengine kuongezwa KACU

March 27, 2025, 9:54 am

Mbunge wa Jimbo la Kahama mjini Jumanne Kishimba akiwa anazungumza katika mkutano mkuu wa 29 wa KACU. (Picha na Sebastian Mnakaya)

Wakulima wengi walioko kwenye chama kikuu cha ushirika wilaya ya Kahama (KACU) ni wa pamba na tumbaku, je, wanaolima mazao mengine mnawaweka wapi katika ushirika huo”

Na Sebastian Mnakaya

Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga (KACU) kimeshauriwa kuongeza mazao mengine mapya yenye tija tofauti na yaliopo sasa ili kuwainua wakulima kwa kuongeza vipato vyao.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Kahama mjini Jumanne Kishimba, wakati wa mkutano mkuu wa 29 wa mwaka wa KACU uliofanyika katika Manspaa ya Kahama, ambapo amesema kuwa katika ushirika kuna mazao mawili Pamba na Tumbaku na kuomba kuongezwa na mazao mengine ili wakulima wanufaike na ushirika wao.

Kishimba amesema KACU inahusisha mazao mawili ya pamba na tumbaku na kuomba mazao mengine ya biashara yaingie ili wakulima wa mazao tofauti na hayo waweze kunufaika na ushirika huo kwa kupata soko la uhakika.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Kahama mjini Jumanne Kishimba

Aidha katika hatua nyingine Kishimba amesema kuwa umefika muda wa wakulima kuanza kulima mazao yenye gharama nafuu na kwenye soko yanauzika kwa haraka na bei kubwa, huku akiomba wataalum kufanya utafiti juu kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao katika sekta ya kilimo.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Kahama mjini Jumanne Kishimba
Mwenyekiti wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika wilaya ya Kahama (KACU) Emmanuel Nyambi

Nae mwenyekiti wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika wilaya ya Kahama (KACU) Emmanuel Nyambi amesema jambo hilo wamelipokea na watalifanyia kazi kwa ushirikiana na wataalam, huku katibu wa AMCOS Segese Mwaja Doto ameomba serikali kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali kuangalia mazao ambayo yataingia katika ushirika tofauti na pamba na tumbaku.

Sauti ya mwenyekiti wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika wilaya ya Kahama (KACU) Emmanuel Nyambi na katibu wa AMCOS Segese Mwaja Doto

Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kina utaratibu wa kila mwaka kufanya mkutano mkuu na wanachama wao kujadili mambo mbalimbali ya ushirika na ukiwa huu ni mkutano wa 29.