

March 24, 2025, 3:58 pm
Wakulima wa zao la pamba na tumbaku wametakiwa kusimamia ubora wa mazao hayo kuanzia shambani hadi katika masoko.
Sebastian Mnakaya
Wakulima wa zao la pamba na tumbaku wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kusimamia vyema ubora wa mazao yao kuanzia katika uzalishaji hadi kuingia sokoni ili kuwa na ubora unaotakiwa.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita wakati wa mkutano mkuu wa 29 wa mwaka wa Chama Cha Ushirika Kahama (KACU) uliofanyika katika manispaa ya Kahama, ambapo amesema kuwa kuzalisha mazao yaliyo bora itawasaidia kuongeza vipato vyao.
Mhita amewataka kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano ili kila mkulima kunufaika na ushirika huo, huku wakitakiwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu ili kuondoa migogoro isiyokuwa na ulazima.
Aidha Mhita amesema umefika wakati wa wakulima kulima kilimo cha biashara chenye tija ili kuondokana na hali ya umasikini kwa kuongeza vipato kupitia kilimo hicho, huku serikali ya awmu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassani ikiendelea kuweka mazingira rafiki katika sekta kilimo.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Mrajisi Msaidizi wa mkoa wa Shinyanga Kakozi Ibrahim amesema ili kuondokana na migogoro mbalimbali katika ushirika ni kufuata maadili, miongozo, sheria na kanuni zilizowekwa katika uongozi kuanzia kwa wanachama wa kawaida wa vyama mbalimbali vya msingi (AMCOS).
Ibrahim amewasihi viongozi wa vyama vya ushirika kujiandaa kuendesha shughuli zao kwa njia ya kidikitali na kuzingatia mabadiliko ya tabianchi ili kuepuka hasara na uhakikisha wanachama wanafaidika.