Wananchi mkoani Shinyanga wametakiwa kupima afya zao mara kwa mara
January 23, 2025, 10:56 am
Katika kipindi cha mvua , baadhi ya wananchi hutiririsha maji taka hali inayosababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko hivyo wazingatie kanuni na taratibu za afya.
Wananchi mkoani Shinyanga wametakiwa kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara pamoja na kutunza mazingira na kutumia maji safi na salama ili kuondokana na magonjwa ya mlipuko.
Agizo hilo limetolewa na kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Faustine Mulyutu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, ambapo amesema kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa na utamaduni wa kupima afya.
Dkt Mulyutu amewataka pia kuwa na tabia ya kufanya usafi katika mazingira yao hususan katika kipindi hiki cha mvua ili kuondokana na changamoto ya magonjwa ya mlipuko ambayo yana athari kwa wananchi.
Naye, diwani wa kata ya Kahama mjini Hamidu Juma amesema katika maeneo yenye hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko ni katika mikusanyika ya watu wengi ikiwemo masoko, na stendi ambapo amewataka kuzingatia kanuni za afya ili kusitokee magonjwa hayo ya mlipuko.