Watoto walindwe dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia
June 18, 2024, 5:07 pm
Kauli mbiu ya mwaka huu ni Siku ya Mtoto wa Afrika ni “Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi”
Na Leokadia Andrew
Wananchi wa manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuendeleo kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria kwa baadhi ya watu wanaowabebesha mimba na kuwakatisha masomo yao.
Kauli hiyo imetolewa na naibu meya wa manispaa ya Kahama Sindano William ambaye pia ni mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa afrika kwa Kahama yamefanyika june 15, 2024, ambapo amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwapa elimu yenye maadili mema ili kumjengea mtoto kifikra pamoja na kuondokana na vitendo viovu kwa watoto.
Akisoma risala katika maadhimisho hayo kwa niaba ya watoto wa wilaya ya Kahama Simon Emmanuel, amesema wazazi na walezi wengi wamekuwa hawawajibiki kwa watoto wao katika maelezi na matunzo, huku wakiomba serikali kuwaajibisha wazazi hao ili waweze kuwajibika kwa watoto wao.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na walezi wilayani humo wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema kuwa wazazi na walezi wasiwe wagumu kuwasaidia mahitaji muhimu watoto wao ili kuwaepushaa kuwakatisha masomo kwa kubeba mimba za utotoni pamoja na kuwalinda na vitendo viovu.
Maadhimisho ya mtoto wa afrika hufanyika kila mwaka ya juni 16 na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili, na stadi za kazi”, ambapo kwa manispaa ya kahama yamefanyika June 15 2024.