NAFASI YA WATAALAM WA MAENDELEO YA JAMII KATIKA ZOEZI LA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022.
April 22, 2022, 2:17 pm
Na Dr. Regina Malima (PhD)
1.0 Utangulizi
SENSA ya watu na makazi ni zoezi maalum lenye lengo la kukusanya na kuchambua takwimu za idadi ya watu katika nchi husika kwa kuangalia umri, jinsia zao, anuani za makazi, kiwango cha elimu, ajira, shughuli mbalimbali za watu, taarifa za vizazi na vifo ili kufanya tathmini na kupanga mipango ya maendeleo kulingana na vyanzo vya mapato vilivyopo.
Katika zoezi la sensa, takwimu za mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hupatikana na hivyo kurahisisha uandaaji wa Sera na Mipango ya Maendeleo kulingana na ulinganifu wa makundi husika katika jamii kwa kuzingatia uhitaji na mazingira yaliyopo.
Nchini Tanzania, Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi muhimu la kitaifa likisimamiwa na Sheria ya Takwimu Sura ya 351 ya mwaka 2019. Zoezi hili hufanyika kila baada ya miaka 10. Sensa zilizowahi kufanyika katika nchi yetu ni pamoja na sensa ya mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012. Sensa ya mwaka huu 2022 itakuwa ni ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 chini ya uratibu wa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Kamati ya Taifa ya Sensa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan mnamo Septemba 14, 2021 alizinduzi rasmi Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa kauli mbiu isemayo “Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa”.
Pia katika uzinduzi huo, Kitabu cha Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kamati ya Taifa ya Sensa kilizinduliwa ikiwa ni maandalizi ya kuelekea zoezi la sensa ya watu na Makazi 2022.
Katika hafla hiyo Mh. Rais alisisitiza wadau wote kwa nafasi zao kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu.
Mh. Rais amefanya jitihada kubwa katika kuonyesha njia kama kiongozi wa nchi kwa kuzindua mkakati huo wenye lengo la kuhamasisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ili Serikali ipate takwimu sahihi zitakazoisaidia kuandaa mipango ya nchi na kufanya maamuzi ya rasilimali na namna ya kupeleka huduma za Kijamii na maendeleo ikiwemo Elimu, Afya, Miundombinu kulingana na idadi kwa wananchi wake.
Mnamo tarehe 08 April 2022 Mh. Rais Samia pia alizindua Nembo na Tarehe ya kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi ambapo itaanza kutumika baada ya kutangaza kuwa Sensa hiyo itafanyika rasmi kuanzia tarehe 23 Agosti 2022 kwa nchi nzima.
Katika hafla hiyo Mh. Rais aliendelea kuagiza na kuwasisitiza Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa ambae ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano waTanzania Mh. Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. John Jingu juu ya maandalizi ya Sensa ikiwemo matumizi ya nembo ya sensa kwa Taasisi za serikali na binafsi ili iweze kuonekana kwa umma.
Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni mtambuka na linahusisha wadau wengi. Sambamba na uandaaji wa mikakati ya uhamasishaji na uelimishaji, ushiriki wa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kama wadau na wahamasishaji wakuu wa shughuli mbalimbali za maendeleo unahitajika katika zoezi la sensa na ni muhimu kujipanga mapema katika ngazi zote ambako wataalamu hawa wamekuwa wakikutana na wananchi moja kwa moja katika shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2022.
2.0 Nafasi ya Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii katika zoezi la Uhamasishaji wa Sensa ya watu na makazi
Maendeleo ya jamii ni mchakato wa kuwajengea uwezo wanajamii ili waweze kujiamini na kuwa na uwezo wa kujituma na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa misingi ya kubaini mahitaji yao, kujua changamoto zinazowakabili, kubuni, kuandaa, kutekeleza, kusimamia na kutathmini mipango ya kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa kutumia kikamilifu raslimali zilizopo.
Maendeleo ya Jamii kama Taaluma ina Wataalam wake wanaofanya kazi na jamii ambao mara nyingi huitwa Maafisa Maendeleo ya Jamii. Kulingana na Mwongozo wa Majukummu ya Wataaalam wa Maendeleo ya Jamii (2019), wataalam hawa wanazo stadi za kutumia mbinu shirikishi zinazowezesha kuamshaari ya jamii kushiriki katika maendeleo yao ikihusisha watu wote na makundi mbalimbali katika jamii.
Stadi hizo ni pamoja na kuelimisha, kuhamasisha na kuraghibisha jamii katika kujiletea maendeleo. Hivyo Wataalam wa maendelo ya jamii wana nafasi kubwa sana ya kufanya uhamasishaji kuelekea zoezi la sensa ya watu na makazi ili kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo la kitaifa litakalonyika mwezi Agosti 2022.
Maendeleo ya Jamii yana uhusiano wa moja kwa moja na takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi kwa sababu maendeleo ni watu.
Na ili watu waweze kupata maendeleo ni muhimu sana idadi yao, umri na jinsia zao, anuani za makazi yao, hali yao ya elimu, hali ya ajira na shughuli mbalimbali wanazozifanya, hali yao ya vizazi na vifo vikajulikana ili uchambuzi yakinifu ufanyike katika kuandaa mipango stahiki, yenye uwiano, yenye ubora na endelevu kufanyika ili kuleta maendeleo na kuboresha maisha yao katika nchi.
Maendeleo ya Jamii yanaenda sambamba na kazi kubwa wanayoifanya Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii nchini katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili kujiletea maendeleo yao wenyewe.
Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii nchini kwa sasa wanafanya kazi katika ngazi za mikoa, Halmashauri/Manispaa/Wilaya, kata na hata vijiji na pia katika asasi mbalimbali za kiraia na sekta binafsi katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo.
Dhamira kuu na msingi wa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni kuongeza ushiriki wa watu katika program mbalimbali za maendeleo ya jamii kama msingi na chachu ya kuwahamasisha kuwa sehemu ya utekelezaji wa program hizo.
Kwa maana hiyo, uhamasishaji wa wananchi kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi ni sehemu ya majukumu ya wataalam wa maendeleo ya Jamii ili kuleta hamasa ya wananchi ili waweze kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kikamilifu.
3.0 Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa Maendeleo ya Jamii
Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi kwa maendeleo ya jamii ni pamoja na:-
1. Sensa ya watu na makazi husadia Serikali kupata takwimu za msingi za nchi kwa sekta zote ikiwemo kujua idadi ya watu wote na ongezeko lake na hivyo kuwezesha serikali kuandaa mipango mbalimbali kisekta na ya kimkakati ya maendeleo ya jamii kwa taifa mfano utekelezaji wa Dira ya Maendeleo Taifa ya mwaka 2025 na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kimataifa na ufuatiliaji wake.
2. Takwimu za idadi ya watu kutokana na sensa zinasaidia mamlaka mbalimbali katika ngazi ya kitaifa hadi kijiji katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya jamii ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika.
3. Taarifa kutokana na Sensa inasaidia upatikanaji wa taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi na hivyo kubaini idadi ya watu kutokana na makundi yao wakiwemo wanaume, wanawake, wazee, watoto, vijana, walemavu, wastaafu n.k kuweza kuwekewa mipango stahiki na endelevu ya maendeleo ya jamii na kiuchumi katika ngazi zote ili kuweza kuboresha maisha yao.
4. Takwimu za sensa husaidia wadau mbalimbali ikiwemo serikali, NGOs, Taasisi za utafiti, watafiti, Taasisi za watu binafsi, Taasisi za elimu ikiwemo vyuo vikuu, na wadau mbalimbali wa maendeleo kutumia taarifa hizo katika mipango na mikakati yao kama msingi wa kuboresha na kupanua shughuli mbalimbali za maendeleo.
5. Takwimu za sensa ya watu na makazi ni za muhimu sana katika masuala ya Maendeleo ya Jamii kwa sababu takwimu hizo husaidia katika kubuni miradi, upangaji na utekelezaji wa program mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kuanzia ngazi ya chini hadi taifa na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika maeneo ya afya, elimu, makazi n.k.
6. Takwimu zitokanazo na Sensa huchangia katika uboreshaji wa maisha ya Watanzania kwa kutoa Takwimu sahihi na zinazoendana na wakati kwa ajili ya kupima kiwango cha maendeleo kilichofikiwa ili kuandaa sera na mipango ya maendeleo ya jamii kwa kipindi kinachofuata.
7. Matokeo ya sensa, yatatoa takwimu muhimu ambazo zitatumika katika uchambuzi wa mabadiliko yaliyopo kuhusu mgawanyiko wa watu ki-umri, mtawanyiko na ongezeko la watu nchini. Hii itawezesha kuainisha maeneo ambayo yatahitaji kufanyiwa utafiti wa kina ili kuweza kujua chanzo cha hali iliyopo na hivyo kuboresha maendeleo ya jamii kwa kutatua changamoto halisi za maisha ya watu katika maeneo husika.
8. Takwimu zitokanazo na Sensa zikitumika vizuri zitasaidia katika kubainisha idadi ya watu wanaoweza kulipa kodi katika nchi na hivyo serikali kupitia mamlaka husika kuweza kukadiria kiasi cha mapato yanayoweza kupatikana kutokana na sekta ya kodi.
4.0 HITIMISHO
Nafasi ya Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni muhimu sana katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa sababu Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ni wahamasishaji na waelimishaji wakuu wakiwa na stadi za kutumia mbinu shirikishi mbalimbali zinazowezesha kuamsha ari ya jamii yote kushiriki katika maendeleo yao, yakiwemo na makundi mbalimbali katika jamii katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Stadi hizo ni pamoja na kuelimisha, kuhamasisha na kuraghibisha jamii katika kujiletea maendeleo.
Hivyo ushiriki wa wataalam wa maendeleo ya jamii katika kuhamasisha wananchi katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti 2022 ni muhimu.
Kwa maana hiyo, sambamba na Kamati ya Taifa ya Sensa na Uandaaji wa Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji kwa ajili ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, ushiriki wa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kama wadau na wahamasishaji wakuu wa shughuli mbalimbali za maendeleo unahitajika katika zoezi hili ili kusafisha njia itakayo amsha ari na hamasa ya wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 2022.