Kahama:wakurugenzi kusimamia mabaraza ya wazee.
October 2, 2021, 2:34 pm
Serikali mkoani Shinyanga imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote sita kuhakikisha wanasimamia na kuyawezesha mabaraza ya wazee ili yaweze kufanya kazi kikamilifu pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shuguli za wazee.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga DK. PHILEMON SENGATI katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika kimkoa katika kata ya Nyandekwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga,
Dk. SENGATI amesema serikali inawatambua wazee kama kundi maalumu linalotegemewa kwa mawazo,hekima na busara kwa maendeleo ya taifa.
Aidha SENGATI amewashukuru wazee kwa kuendelea kuwa wahamasishaji na kuchukua chanjo ya uviko 19, huku akiahidi kuwachukulia hatua wanaopotosha kuhusu chanjo hiyo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kahama FESTO KISWAGA amesema serikali wilayani Kahama itahakikisha kuwa wazee pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi wanalindwa dhidi ya ukatili.
Naye Mweyekiti wa baraza la wazee mkoa wa Shinyanga FAUSTINE MASALE ameiomba serikali kuendelea kuunga mkono na kusaidia mabaraza ya wazee,huku akisema kwamba ukatili dhidi ya wazee umepungua kwa kiasi kikubwa katika mkoa wa Shinyanga.
Oktoba mosi Kila mwaka dunia huadhimisha siku ya wazee duniani, ambapo kwa mwaka huu Kaulimbiu ya maadhimisho hayo matumizi sahihi ya kidigitali kwa ustawi wa rika zote.