KAHAMA:DC awashukia TARURA ubovu wa barabara ya kusafirisha Mchele.
September 1, 2021, 12:32 pm
Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga amemwaagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kuzungukia barabara zote zilizo chini yao za mitaa na vijiji ili kubaini maeneo yenye ubovu wa barabara na kuyafanyia marekebisho.
Kiswaga ametoa agizo hilo leo alipotembelea barabara ya Kata ya Malunga mtaa wa Igomelo inayopitisha magari yanabeba mchele kutoka eneo la mashine na kujionea shimo lililo katikati ya daraja linaloleta usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Redio Kahama Fm kutoa taarifa ya ubovu wa barabara hiyo hali inayosababisha wasafirishaji wa mchele kwenda nje ya nchi kupata shida kutokana na barabara hiyo kushindwa kupitika kirahisi.
Katika hatua nyingine Kiswaga ameiagiza kampuni ya Emmegency iliyopewa tenda ya kukarabati barabara hiyo kulifukia shimo hilo ili magari yaanze kupita na ametoa maelezo kwa TARULA kuwahimiza watu wanaosaini mikataba ya kazi kuanza kazi kwa wakati.
Kwa upande wake meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Wilaya ya Kahama Joab Mutagwaba amewataka madereva kutokuwa na wasiwasi na kwamba wataonyeshwa barabara mbadala ya kutumia wakati mkandarasi akiendelea kufanya marekebisho.
Naye meneja wa kampuni ya Emmegency Response Fabiani Paschal amesema kuwa ameyapokea na atayafanyia kazi maagizo ya mkuu wa Wilaya na kuongeza kuwa changamoto ya barabara hiyo ni kupita magari yenya uzito mkubwa zaidi ya Tani 10.