Madiwani wa halmashauri ya Msalala wilayani Kahama waomba serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba.
August 30, 2021, 12:41 pm
Madiwani wa halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameiomba serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba pamoja na dawa katika vituo vya afya pamoja na zahanati, ikiwemo zahanati ya Bugarama.
Madiwani hao wamesema hayo katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya nne, ambapo wamesema kumekuwepo na changamoto kwa kinamama wajawazito wanaokwenda kupata huduma, kukosa vifaa hivyo pamoja na dawa hali hiyo inayosababisha wananchi kutumia gharama zao kwa ajili ya kununua vifaa pamoja na dawa.
Kwa upande wake kaimu Mganga mkuu wa Halmashauri hiyo, IGNAS KAFULILA amesema kuwa kwa mujibu ya sheria ya afya ya mwaka 2007 imeeleza kuwa mama mjamzito anatibiwa bure kwa kipindi chote cha ujauzito hadi anapojifungua.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala CHARLES FUSSI amewataka watumishi wa idara ya afya kuwa na lugha nzuri pindi wanapowahudumia wagonjwa pamoja na kutoa maelezo ya kutosha pindi dawa zinapokosekana katika zahanati na vituo vya afya.