TBS
Kahama FM

TBS yatoa Elimu kwa wasindikaji wa Mchele Kahama.

April 28, 2021, 7:06 am

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu kwa wasindikaji, wajasiriamali na wadau wa mchele wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga katika mnyororo wa thamani kuhusu kanuni bora za uzalishaji,matakwa ya viwango,namna bora ya uhifadhi,elimu juu ya vifungashio na taarifa za msingi zinazotakiwa kuwepo kwenye vifungashio.

Meneja wa Utafiti na Mafunzo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw.Hamisi Sudi 

Mafunzo hayo yamefanyika leo Jumanne Aprili 27,2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na kukutanisha wajasiriamali 100 wanaojihusisha na bidhaa ya Mchele ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha aliishukuru TBS kwa kukutana na wasindikaji, wajasiriamali na wadau wa mchele akieleza kuwa ni kundi la wajasiriamali ambao ni sehemu muhimu katika sekta binafsi inayochangia pato la taifa,kuongeza ajira na kuondoa umaskini nchini.

Licha ya kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia ubora,viwango na usalama pia aliwakumbusha kuwa waaminifu kwa wateja wao kwa kuepuka  kuchanganya mchele kutoka maeneo tofauti na kuuza kwa bei juu.

Aidha aliwasihi wafanyabiashara wa mchele kuwa wazalendo na kuepuka kushirikiana na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wanaokuja na vifungashio vyao na kutambulisha mchele wa Tanzania kuwa unazalishwa katika nchi hizo akibainisha kuwa kitendo hicho ni kuhujumu uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Meneja wa Utafiti na Mafunzo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw.Hamisi Sudi Mwanasala alisema TBS inataka bidhaa nzuri zifungwe kwenye vifungashio sahihi zikiwa na taarifa sahihi ili kulinda afya za watumiaji.

Alisema TBS inaendelea kutoa elimu kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa wanapata elimu na utaalamu kuhusu kanuni bora za uzalishaji, matakwa ya viwango,namna bora ya uhifadhi,elimu juu ya vifungashio na taarifa za msingi zinazotakiwa kuwepo kwenye vifungashio ili kuleta ushindani na kukuza uchumi wa nchi.

Mafunzo hayo yameandaliwa na TBS kama moja ya utekelezaji wa makubaliano ya kikao cha wadau katika mpaka wa Sirari ambacho kiliadhimia TBS kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wasindikaji na wadau wa mchele katika Kanda ya Ziwa.

Wasindikaji, wajasiriamali na wadau wa mchele wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga wakiwa ukumbini wakifuatilia mafunzo kuhusu kanuni bora za uzalishaji