Wadau Shinyanga walia na Shria ya ndoa ya Mwaka 1971 ya binti kuolewa akiwa na miaka 14.
April 15, 2021, 4:15 pm
SHERIA ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi, na 15 Mahakama, imetajwa kuwa tatizo kukomesha mimba na ndoa za utotoni.
Mkurugenzi wa Shirika la Agape linalotetea haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga, John Myola alibainisha hayo jana kwenye ziara ya machampion wa kupambana na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, walipotembelea watoto ambao ni wahanga wa matukio hayo katika Shirika la Agape, ziara iliyoandaliwa na Shirika la Msichana Intiative.
Amesema moja ya changamoto kubwa ambayo wanakabiliana nayo katika mapambano ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga, ni Sheria hiyo ya ndoa ya mwaka 1971, ambayo imekuwa ikisababisha wahusika kutofungwa jela na kuwa fundisho kwa wengine sababu ya kuruhusu mtoto chini ya miaka 18 kuolewa.
Naye mmoja wa machampion, Aida Kenani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini , amesema kuna haja kubwa ya Sheria hiyo ya ndoa kufanyiwa marekebisho ya haraka ili kumlinda mtoto wa kike kutimiza ndoto zake.
Aidha akizungumza na watoto ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni wanaolelewa na Shirika la Agape, amewataka wasikate tamaa, bali wasome kwa bidii ili watimize ndoto zao ambazo zilizotaka kuzimwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeka Gyumi, ambao wanatetea haki za watoto, amesema wamefanya ziara hiyo na machampion ili kujifunza, kubadilisha uzoefu na kuchukua changamoto, ambazo ni tatizo kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, ili ziendelee kutafutiwa ufumbuzi.
Pia amewataja machampion wengine wa kupambana kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ambao aliaambatana nao, kuwa ni Mbunge mwakilishi wa vijana taifa kutoka mkoani Mwanza, Ng’wasi Kamani na aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2005 Nancy Sumari pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Waislamu Tanzania, Shamimu Khan.