Adhana FM

Wadau wa utalii Zanzibar wametakiwa kubuni mbinu mpya za kuwavutia watalii

17 October 2021, 4:22 pm

Na Kassim Abd OMPR

Makamo wa pili wa rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka wadau wa utalii kubuni mbinu mpya zitakazoleta ushindani kwa kuibua vivutio vipya sambamba na kuviimarisha vivutio vyengine ili viwe na mazingira yatakayowashawishi watalii kurudi tena kuitembelea Zanzibar.

Hemed alitoa witò huo wakati akilifungua kongamano la wadau wa utalii Zanzibar lililofanyika katika Hotel ya Golden Tulip Airport Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais alibainisha kwamba, wadau wa utalii wasirizike na dhana kuwa Zanzibar inajitangaza yenyewe bali inapaswa kuchukua jitihada za maksudi ili kuingia katika ushindani kutokana na nchi nyengine kuendelea kuchukua hatua mbali mbali za kutangaza nchi zao.

Aidha, makamo wa pili wa rais aliupongeza uongozi wa Jumuiya ya Kitaifa ya wafanyabiashara Zanzibar kwa kushirikiana na UNDP kwa hatua wanazozichukua katika kurudisha ustawi wa sekta ya utalii Zanzibar kwa ajili kuinua uchumi wa Nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya kitaifa ya wafanyabiashara Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa katika mwaka 2020 sekta ya utalii ilitarajiwa kuchangia pato la taifa (GDP) kwa asilimia Thelasini na Tano (35%) pia ilitarajiwa kukusanya asilimia Themanini (80%) ya mapato pamoja na kuajiri watu wapatao laki moja (100,000) lakini kutokana na janga la UVIKO_19 lilisababisha kushindwa kufikiwa kwa lengo hayo.

Nae, Mwakilishi kutoka UNDP, Rukia Wadoud alisema UNDP inaipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano wake inautoa kwa kuwashirikisha wadau kutoka taasisi binafasi na kuahidi kuwa UNDP itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa serikali ili kuinua maendeleo ya sekta ya utalii Zanzibar.