Wafanyabiashara endeleeni kulipa kodi-ZRA
15 June 2024, 12:47 pm
Nimuhim kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Na Abdul Sakaza.
Mamlaka Ya Mapato Zanzibar (ZRA) imewataka wananchi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuendelea kulipa kodi ili kuongeza pato la taifa.
Ameyasema hayo Meneja wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Kikodi kutoka Mamlaka Ya Mapato Zanzibar (ZRA) Hanii Mohamed Khamis wakati alipokua akizungumza na Wananchi na wafanyabiashara wa Mkoa huo kupitia kipindi maalum cha Radio Jamii Tumbatu FM.
Meneja Hanii, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kulipa kodi ikiwemo kuongeza pato la Taifa ambalo huchangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga miundombinu mbali mbali ya kijamii ikiwemo Barabara, Vituo vya Afya, Shule pamoja na Masoko ambayo husaidia ukuaji wa maendeleo Nchini
Katika hatua nyengine amewataka Wanachi na wafanyabiashara kudai risiti za kielektroniki wanaponunua bidhaa mbali mbali na kuacha kupokea risiti za kienyeji zinazoandikwa kwa mikono ambazo zimepigwa marufuku na Serikali Ya Mapinduzi Ya Zanzibar kutumiwa na Wafanyabiashara
Kwa upande wake Afisa elimu kutoka Mamlaka Ya Mapato Zanzibar (ZRA) Ndugu, Abdulshakur Ramadhan Simai ameweka bayana kua kwasasa wameazisha programu(APP) maalumu inayopatikana Play Store inayojulikana “ZRA FUNGUKA” ili kurahisisha kupokea maoni kwa wananchi na wafanyabiashara hapa nchini
Nao Wananchi na Wafanyabiashara wa Mkoa huo walioshiriki kipindi hicho kwa njia ya simu Kupitia Radio Tumbatu FM wameishukuru Mamlaka Ya Mapato Zanzibar( ZRA ) kwa kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kudai risiti za kielektroniki kwani walikua hawana elimu hiyo na wameahidi kuifanyia kazi elimu hiyo walioipata.